Maajabu ya teknolojia yanaendelea kugusa maisha ya watu kwa namna isiyotarajiwa. Fikiria uko kwenye chumba kimoja na wapendwa wako, unawasikia wakicheka na kuongea, lakini huwezi kugeuza kichwa chako kuwaangalia. Huu ndio ulikuwa ukweli mchungu wa Brad Smith, baba aliye na ugonjwa wa kupooza misuli ujulikanao kama ALS (uleule uliomuua mwanafizikia maarufu Stephen Hawking). Kwa miaka saba, Brad amekuwa amefungwa kwenye kiti cha magurudumu, hawezi kuongea wala kutikisa kiungo chochote.
Lakini mwanga mpya uliangaza maishani mwake mwezi Novemba mwaka jana alipokuwa mtu wa tatu duniani kupandikizwa 'chip' ya kompyuta kwenye ubongo wake na kampuni ya Neuralink ya bilionea Elon Musk. Hatua hii ya kwanza ilimwezesha kutumia kompyuta kwa mawazo yake tu na hata 'kuongea' tena kupitia sauti bandia iliyotengenezwa na Akili Mnemba (AI). Sasa, Brad amepiga hatua nyingine kubwa zaidi; amepata "macho mapya".
Kupitia filamu fupi ya dakika nane iitwayo 'A Second Pair of Eyes' (Jozi ya Pili ya Macho), Brad anaonyesha jinsi kamera ndogo ya kisasa kutoka kampuni ya Insta360 ilivyombadilishia maisha. Kwa msaada wa wahandisi, kamera hii iliunganishwa na kompyuta yake na mfumo unaofuata mwendo wa mboni zake za macho. Matokeo yake ni ya kustaajabisha: sasa anaweza 'kugeuza' kamera hiyo kwa kutumia macho yake tu, akiiangalia familia yake ikicheza, kana kwamba anageuza kichwa chake mwenyewe.
Kwenye video hiyo inayoliza kwa furaha, Brad anaonekana akifuatilia michezo ya wanae kwa kutumia 'jicho' lake hili jipya la kielektroniki. "Nilikuwa nimefungwa kwenye dunia iliyosimama, wakati maisha ya familia yangu yakiendelea kwa kasi," anasimulia kwa kutumia sauti yake ya AI. "Kitu kilichoniuma zaidi ni kutoweza kuwaangalia machoni wanangu wanapoongea nami."
Sasa, shukrani kwa mchanganyiko wa teknolojia ya Neuralink na kamera hiyo ya AI, Brad siyo tu baba anayekaa kimya kwenye kona.
Amerudi kuwa mshiriki hai wa familia, anaweza kurekodi matukio muhimu, na hata kutengeneza video zake mwenyewe za YouTube. Teknolojia imempa zaidi ya uwezo wa kuona; imemrudishia nafasi yake kama baba na msimulizi wa hadithi za familia yake.