Amazon Yafanya Kufuru Las Vegas: Yazindua 'Nova 2' na Kumpa Mfanyabiashara Uwezo wa Kuunda Roboti Yake Mwenyewe

it | Thu Dec 04 2025


Amazon Yafanya Kufuru Las Vegas: Yazindua 'Nova 2' na Kumpa Mfanyabiashara Uwezo wa Kuunda Roboti Yake Mwenyewe

Katika kile kinachoonekana kama "kutikisa kiberiti" katika ulimwengu wa teknolojia, kampuni tanzu ya Amazon inayojihusisha na huduma za mtandao, Amazon Web Services (AWS), imeamua kuwavulia kofia washindani wake kama Google na Microsoft. Kwenye mkutano wao mkubwa wa mwaka ujulikanao kama AWS re:Invent unaofanyika Las Vegas, Marekani, Amazon imetangaza mapinduzi makubwa kwa kuzindua kizazi kipya cha Akili Mnemba (AI) kinacholenga kumfanya kila mfanyabiashara awe "Bosi wa Teknolojia."


Kivutio kikubwa hakikuwa tu roboti mpya, bali ni huduma mpya iitwayo ‘Nova Forge’. Huduma hii ni kama karakana maalum inayomwezesha mfanyabiashara kuchukua teknolojia ya Amazon na kuichanganya na data zake za siri ili kutengeneza roboti yake binafsi anayoitaka yeye.


Familia Mpya ya 'Nova 2': Kila Mtu na Saizi Yake


Amazon haikuja kinyonge; imemwaga sokoni aina nne za "injini" mpya za AI chini ya mwamvuli wa 'Nova 2', zilizopangwa kulingana na uwezo na kazi:


  1. Nova 2 Lite: Huyu ni "Kibarua Hodari." Ni mfumo mwepesi, wenye kasi ya ajabu na gharama nafuu. Umetengenezwa kushughulikia kazi za kila siku za ofisini. Amazon inadai kuwa katika majaribio, mtambo huu umewapiga 'bao' washindani wake kama GPT-5 mini na Gemini 2.5 kwa ufanisi.
  2. Nova 2 Pro: Huyu ni "Wakili Msomi." Ana akili nyingi za kutatua matatizo magumu, kuandika kodi za kompyuta (coding), na kupanga mikakati ya muda mrefu.
  3. Nova 2 Sonic: Huyu ni "Kasuku." Ni bingwa wa sauti. Ana uwezo wa kuongea na binadamu kwa lugha mbalimbali huku akionyesha hisia na kubadili mada kama unavyopiga stori na mshikaji wako kijiweni.
  4. Nova 2 Omni: Huyu ndiye "Mtaalamu wa Yote." Ana uwezo wa kuchakata maandishi, picha, video, na sauti kwa mpigo. Anaweza kusoma nyaraka ndefu, kusikiliza sauti za masaa mengi, na kuangalia video kwa wakati mmoja na kukupa majibu.


Matt Garman, Mkurugenzi Mtendaji wa AWS, amesema: "Nova 2 Lite itakuwa punda wa mzigo (workhorse) kwa makampuni mengi, wakati Pro ni kwa wale wanaotaka mambo makubwa zaidi."


Nova Forge: "Pika Chakula Chako Mwenyewe"


Hapa ndipo kwenye utamu. Kwa muda mrefu, makampuni yamekuwa yakiogopa kutumia AI za nje kwa hofu ya kuvujisha siri zao. Nova Forge inakuja kama suluhisho. Inampa mteja uwezo wa kuunda modeli yake binafsi inayoitwa ‘Novella’.


Kupitia huduma hii, benki au kampuni ya simu inaweza kuchukua 'akili' ya msingi ya Amazon, ikaichanganya na data zake za wateja (kwa usalama), na kutengeneza roboti inayojua kila kitu kuhusu biashara hiyo pekee. Zaidi ya hayo, wanapewa kitu kinaitwa 'RL GYM'—kama 'Gym' ya mazoezi ambapo roboti hiyo inafundishwa jinsi ya kufanya maamuzi katika mazingira magumu kabla haijaingia kazini.


Bei ya Mkasi: Milioni 270 kwa Mwaka


Teknolojia hii si ya bure. Gharama ya kutumia huduma ya Nova Forge imetajwa kuwa Dola 100,000 kwa mwaka. Ukibadilisha fedha hizi kwa madafu yetu, ni takriban Shilingi Milioni 270 za Kitanzania. Ingawa inaonekana pesa nyingi kwa mjasiriamali mdogo wa Kariakoo, kwa mashirika makubwa kama mabenki na kampuni za mawasiliano, hii ni bei chee ukilinganisha na faida ya kuwa na mfumo unaoendeshwa na data zako mwenyewe.


Tayari makampuni makubwa kama mtandao wa Reddit, Sony, na Booking.com yameanza kutumia huduma hii kuboresha biashara zao.

Kwanini Hawakutoa Matokeo ya Mtihani (Benchmarks)?


Kitu cha kushangaza ni kwamba Amazon haikutoa takwimu za kulinganisha uwezo wa Nova 2 na washindani wake (Benchmarks). Rohit Prasad, Makamu wa Rais wa AGI pale Amazon, alijibu kwa mkato: "Hayo majaribio yamejaa vurugu na uongo. Sisi tumeamua kuleta bidhaa inayofanya kazi, siyo bidhaa ya kushinda kwenye makaratasi."


Kwa Tanzania na Afrika Mashariki, uzinduzi huu unafungua milango kwa makampuni ya 'Fintech' na wabunifu wa 'Silicon Dar' kuanza kufikiria jinsi ya kutengeneza mifumo ya AI inayoelewa Kiswahili na mazingira yetu kwa kutumia data zetu wenyewe kupitia Nova Forge.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.