Mkoa wa Kamchatka, uliopo Mashariki mwa mbali ya Urusi, unaendelea kukumbwa na misukosuko ya kiasili baada ya kutikiswa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.8, ambalo sasa linafuatiwa na matetemeko madogo ya mara kwa mara (aftershocks) na milipuko ya volkano. Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, RIA Novosti, Wizara ya Hali ya Hatari ya nchi hiyo imetangaza kuwa ndani ya siku moja tangu tetemeko kubwa, jumla ya matetemeko 120 madogo, yenye ukubwa kati ya 3.5 hadi 6.7, yametokea katika mkoa huo.
Kutokana na hali hiyo ya hatari, Wizara ya Hali ya Hatari imewataka wananchi na watalii kujiepusha na volkano hatari za eneo hilo, ikiwemo Bezymianny, Shiveluch, Klyuchevskaya na Karimsky, na pia kuepuka kutembelea volkano ya Avachinsky.
Kufuatia tetemeko hilo kubwa la ardhi, lililotokea katika bahari ya Kamchatka mnamo Julai 30, 2025, volkano kadhaa zilianza kuonyesha dalili za kuongezeka kwa shughuli zao. Shirika la Kijiofizikia la Urusi limesema kuwa Klyuchevskaya, volkano yenye urefu mkubwa zaidi katika ulimwengu wa Kaskazini, ilianza kulipuka siku ya tetemeko hilo, na lava nyekundu ilionekana ikishuka kwenye mteremko wake wa Magharibi.
Mtaalamu wa volkano kutoka Kituo cha Ufuatiliaji wa Volkano, Yuri Demyanchuk, amesema ingawa volkano ya Klyuchevskaya ilikuwa tayari inalipuka tangu mwezi wa Aprili, tetemeko la ardhi limechangia kuongeza shughuli zake. Aliongeza kuwa volkano ya Shiveluch pia imeanza 'kuamka' baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, na volkano ya Avachinsky inatoa moshi na gesi, hali inayofanya eneo hilo kuwa hatari.
Kuna hofu pia kuhusu lava kutoka volkano ya Klyuchevskaya ambayo inaelekea kwenye barafu kubwa ya Bogdanovich. Ikiwa lava hiyo itakutana na barafu hiyo, inaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa mvuke na kutengeneza maporomoko ya tope yanayotiririka kuelekea mto wa karibu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press (AP), Kamchatka, ambayo inajulikana kama "Ardhi ya Moto na Barafu," ina takriban volkano 300, ambapo 29 kati ya hizo bado zinawaka. Hali hii inaifanya Kamchatka kuwa moja ya maeneo hatari zaidi duniani kutokana na matukio ya kiasili.