Kuna usemi wa wahenga unaosema "Mti mzuri hukua haraka," lakini kile kinachotokea huko Silicon Valley, Marekani, kimevuka mipaka ya ukuaji wa kawaida na kuingia kwenye maajabu ya kifedha. Kampuni changa kabisa (startup) iitwayo Thinking Machines Lab (TML), ambayo haina hata mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, inatarajiwa kuvunja rekodi zote kwa kufikisha thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 50 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 135) ndani ya muda mfupi mno.
Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika kutoka Bloomberg, TML, ambayo ilianzishwa na vigogo waliojitoa kutoka kampuni maarufu ya OpenAI, ipo katika hatua za awali za majadiliano ya kupokea uwekezaji mpya. Ikiwa dili hili litatiki, litapandisha thamani ya kampuni hiyo mara nne zaidi ya ilivyokuwa mwezi Julai mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa, mwezi Julai, TML iliweka rekodi ya dunia kwa kupata mtaji wa kuanzia (seed funding) mkubwa zaidi katika historia ya Silicon Valley, uliokadiriwa kufikia Dola bilioni 12 (kama TZS Trilioni 32.4). Sasa, miezi minne tu baadaye, wanataka kupaa hadi kufikia thamani ambayo makampuni mengi makongwe yameishia kuisikia kwenye bomba.
Siri ya Utajiri Huu ni Nini?
Mafanikio haya ya haraka hayaji kwa bahati mbaya. TML inaongozwa na Mira Murati, mwanamama ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Teknolojia (CTO) wa OpenAI (wamiliki wa ChatGPT). Kuwepo kwa "bongo" hizi zilizohusika kutengeneza teknolojia zinazotikisa dunia kumeipa kampuni hii hadhi ya kipekee mbele ya wawekezaji.
Bidhaa yao ya kwanza, iliyopewa jina la 'Tinker', tayari imeshaanza kutikisa soko. Hii ni zana maalum inayotumiwa na makampuni makubwa kurekebisha na kuboresha mifumo ya Akili Mnemba (LLMs) ili ifanye kazi kulingana na mahitaji yao maalum (fine-tuning). Tayari, vyuo vikuu vyenye hadhi ya juu duniani kama Princeton na Stanford vimeanza kuitumia na kuisifia, huku wateja wengine wa kibiashara wakianza kulipia huduma hiyo.
Vita ya 'Neolabs'
TML si peke yake. Kumeibuka wimbi jipya la makampuni yanayoitwa 'Neolabs'—hizi ni kampuni mpya zilizoanzishwa na wafanyakazi wa zamani wa OpenAI na Anthropic ambao wameamua kujitegemea. Mfano mwingine ni kampuni ya SSI iliyoanzishwa na Ilya Sutskever (aliyekuwa mwanasayansi mkuu wa OpenAI) na Periodic Labs.
Kufikia thamani ya Dola bilioni 50 kutaiweka TML katika klabu ya kipekee ya matajiri wa teknolojia ambao hawajaingia soko la hisa (private companies). Kwa sasa, ni makampuni machache sana kama OpenAI (yenye thamani ya Dola bilioni 500), Anthropic (Dola bilioni 183), xAI ya Elon Musk (Dola bilioni 50), na Databricks (Dola bilioni 62) ndiyo yamefikia viwango hivi. Hata kampuni maarufu ya utafutaji mtandaoni ya Perplexity, ambayo ina miaka minne sokoni, ina thamani ya Dola bilioni 20 tu—kiasi ambacho ni nusu ya kile TML inachokaribia kukipata ndani ya mwaka mmoja.
Wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema kama hali hii itaendelea, thamani ya TML inaweza hata kugonga Dola bilioni 60 (TZS Trilioni 162). Hii inadhihirisha kuwa 'homab ya dhahabu' katika sekta ya Akili Mnemba bado ni mbichi na wawekezaji wako tayari kumwaga fedha popote wanapoona dalili ya mapinduzi mapya ya kiteknolojia.