"iPhone 17 Bado Haina Akili Mnemba ya Kweli" – Wachambuzi Waiponda Apple

it | Wed Sep 10 2025


"iPhone 17 Bado Haina Akili Mnemba ya Kweli" – Wachambuzi Waiponda Apple

Uzinduzi wa hivi karibuni wa simu janja za iPhone 17 uliofanyika Cupertino, California, umeacha maswali mengi kuliko majibu, huku kampuni ya Apple ikijikuta katika lawama nzito kutoka kwa wachambuzi. Jarida maarufu na lenye mamlaka makubwa la teknolojia nchini Marekani, TechCrunch, limekuwa la kwanza kutoa hukumu kali, likisema wazi: "iPhone 17 bado haina Akili Mnemba (AI)."


Wakati Apple ikijivunia muundo mwembamba wa simu zake mpya, TechCrunch linaonya kuwa zama za kushindana kwa wepesi na unembamba wa simu zimepita. Kwa sasa, vita halisi iko kwenye upande wa programu (software), na hasa, uwezo wa Akili Mnemba. Katika eneo hili muhimu, jarida hilo linasema Apple "imeachwa mbali nyuma na washindani wake."


Ukosoaji unazidi pale ilipobainika kuwa katika uzinduzi mzima, hakukuwa na tangazo lolote kubwa kuhusu maboresho ya AI kama sehemu muhimu ya kuwavuta wateja kununua toleo jipya. Kipengele pekee cha AI kilichotajwa kwa uzito ni uwezo wa kutafsiri lugha kwa wakati halisi unaopatikana kwenye 'AirPods 3', jambo ambalo linaonekana dogo mno ukilinganisha na matarajio ya soko.


Cha kushangaza zaidi, msaidizi wa kidijitali wa Apple, Siri, hakutajwa kabisa, iwe ni katika maboresho ya kawaida au yale yanayohusisha AI. Hali hii imezua mjadala mkubwa kuhusu jinsi "kosa hili la kimkakati la Apple kuhusu AI" linavyoweza kuathiri vibaya sifa ya kampuni na mafanikio yake ya baadaye.


TechCrunch linaweka wazi tofauti kubwa iliyopo kwa kuilinganisha Apple na Google, ambayo mwezi uliopita ilizindua simu yake ya 'Pixel 10' ikiwa imesheheni mfumo endeshi wa Android wenye nguvu ya AI. Wakati watumiaji wa Android wakifurahia ubunifu huu, wateja wa Apple watalazimika kusubiri hadi mwaka 2026 kwa ajili ya toleo la Siri lenye nguvu ya AI.


Jarida hilo linaendelea kusema kuwa hadi sasa, Apple imetoa tu vitu vinavyoweza kuonekana kama "AI ya kawaida" kama vile zana za kuandika, kufupisha maandishi, kutengeneza picha (ambazo baadhi wanalalamika hazina ubora), utafutaji wa picha, na 'Genmoji'. Hivi vyote havitoshi katika ushindani mkali wa sasa.


Mbaya zaidi, kumekuwa na ripoti kwamba Apple sasa inatafuta msaada kutoka kwa makampuni mengine (third-party) ili kuweza kushindana kwenye mbio za AI. Uamuzi huu, kwa mujibu wa TechCrunch, unaweza kuwa "habari mbaya" kwa Apple, kwani inaashiria udhaifu wa ndani na huenda ikalazimu kampuni kutumia fedha nyingi kununua kampuni nyingine ili kuziba pengo.


Mwisho, TechCrunch lilitoa ushauri wa kejeli kwa Apple: "Apple inaweza kuendelea kujitangaza kama mtengenezaji bora wa vifaa (hardware) duniani, lakini si kama kampuni inayoongoza kwa vifaa vyenye Akili Mnemba."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.