Apple Kuleta Mfumo wa AI Kwenye Vision Pro Kuanzia Aprili

it | Mon Feb 24 2025


Apple Kuleta Mfumo wa AI Kwenye Vision Pro Kuanzia Aprili

Apple imetangaza kuwa kuanzia Aprili mwaka huu, watumiaji wa kifaa chake cha mseto wa uhalisia (Mixed Reality), Vision Pro, wataweza kufurahia huduma ya akili bandia (AI) kupitia mfumo wake mpya, Apple Intelligence.


Mfumo huu unakuja na uwezo wa kusaidia katika uandishi wa maandishi kwenye programu kama Mail na Notes. Watumiaji wataweza kuandika na kuhariri maandishi kwa urahisi, kubadilisha mtindo wa uandishi kuwa wa kitaalamu au wa kifupi, pamoja na kusahihisha makosa ya sarufi na mpangilio wa sentensi. Pia, itaruhusu muhtasari wa maandishi marefu na uundaji wa maudhui mapya kupitia ChatGPT.


Katika kipengele cha Image Playground, watumiaji wataweza kuunda picha kwa kuchagua mandhari, mavazi, vifaa vya kuvaa, na maeneo yanayohitajika. Pia, itawezekana kutengeneza picha za katuni kulingana na picha halisi za familia au marafiki. Kipengele kingine, Genmoji, kitawawezesha watumiaji kuunda emoji zao za kipekee na kuzituma kama ujumbe au stika.


Huduma nyingine zinazotolewa kupitia Apple Intelligence ni pamoja na:

  1. Smart Reply – Inatoa mapendekezo ya majibu sahihi kwa ujumbe.
  2. Memory Video Creation – Inachagua picha na video maalum ili kuunda hadithi ya kumbukumbu.
  3. Natural Language Search – Inasaidia kutafuta picha na video maalum kwa kutumia maelezo ya kawaida ya lugha.


Kwa sasa, Apple Intelligence kwenye Vision Pro inapatikana kwa lugha ya Kiingereza pekee, lakini Apple imeahidi kuongeza lugha zaidi na vipengele vipya kabla ya mwaka kumalizika.


Akizungumzia maboresho haya, Makamu wa Rais wa Kitengo cha Vision Products Group, Mike Rockwell, alisema: "Watumiaji sasa wanaweza kutumia zana za uandishi, Image Playground na Genmoji kuinua ubunifu na tija yao katika kiwango kipya."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.