Rais Xi Jinping wa China ameonekana hadharani mara kadhaa hivi karibuni, akiongoza mikutano muhimu, ishara inayoashiria uthabiti wa mamlaka yake kufuatia uvumi uliokuwa ukienea katika baadhi ya vyombo vya habari na majukwaa kama YouTube kuhusu matatizo ya uongozi wake. Mwonekano wake wa mara kwa mara unakwenda kinyume na tetesi hizo, ukisisitiza kuwa bado ana udhibiti kamili wa serikali na chama.
Shirika la habari la serikali ya China, Xinhua, lilifafanua kuwa mnamo Julai 1, 2025, Rais Xi aliongoza mkutano wa sita wa Kamati Kuu ya Fedha na Uchumi. Katika mkutano huo, walijadili masuala mbalimbali, ikiwemo juhudi za kuendeleza ujenzi wa "soko la kitaifa lililounganishwa." Dhana hii ni sehemu muhimu ya mkakati wa "mzunguko pacha" wa China, unaolenga kukuza uchumi wa ndani na kufanya mageuzi ya kitaifa ili kuimarisha mzunguko wa ndani. Serikali ya China imekuwa ikifanya kazi ya kuondoa vikwazo vya kiutawala na kimfumo vinavyozuia ujenzi wa soko la ndani lililounganishwa kitaifa.
Katika mkutano huo, walisisitiza mbinu ya "umoja 5 na uwazi 1." Hii inamaanisha kuunganisha mambo matano muhimu: mifumo ya msingi ya soko, miundombinu, viwango vya utendaji wa serikali, usimamizi wa soko, na soko la rasilimali za uzalishaji. Sambamba na hayo, wataongeza uwazi katika masoko ya ndani na nje. Mbali na hayo, serikali iliahidi kudhibiti ushindani usio na utaratibu unaosababishwa na bei za chini zisizo halali kutoka kwa makampuni, na kuwezesha kuondoka kwa utaratibu kwa wazalishaji wasio na tija. Hatua hizi zinafanana na juhudi za serikali ya Tanzania za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza ushindani wa haki.
Siku moja kabla ya kuadhimisha miaka 104 ya kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China (Julai 1), Rais Xi pia alishiriki katika kikao cha pamoja cha masomo cha Politburo ya Kamati Kuu ya Chama. Televisheni Kuu ya China (CCTV) ilionesha Rais Xi akiongoza kikao hicho, akishirikiana na viongozi wengine wa ngazi za juu. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kupambana na rushwa.
Rais Xi alionya kuwa "mazingira ya uongozi yanayokabili chama chetu ni magumu sana." Aliwakumbusha wanachama na viongozi wa chama, bila kujali nafasi zao, kuwa na wajibu wa "kujipiga vita wenyewe" dhidi ya rushwa, huku akisisitiza kuwa viongozi waandamizi wanapaswa kuwa mfano bora katika kujirekebisha. Zaidi ya hayo, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uaminifu na uadilifu wakati wa uteuzi wa vipaji vipya. Alisema, "Katika vita dhidi ya rushwa, ni lazima kuweka viwango vya uendeshaji wa mamlaka, kuunda muundo ulio wazi na unaoweza kufuatiliwa, na kutafuta mianya katika uendeshaji wa mamlaka." Katika mkutano huo wa Politburo, pia walipitia "Kanuni za Kazi za Vyombo vya Kuratibu Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama."