Kundi la Wahouthi nchini Yemen limedai kurusha makombora ya balistiki kuelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion ulioko katikati mwa Israel na mji wa Tel Aviv. Shirika la habari la China, Xinhua, na shirika la habari la Marekani, AP, vimeripoti tukio hilo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa Wahouthi, Yahya Sarea, kundi hilo lilirusha makombora mawili ya balistiki kulenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion na kambi ya kijeshi iliyoko Tel Aviv.
Sarea aliongeza kuwa walianzisha mashambulizi kwa kutumia makombora ya balistiki, makombora ya cruise, na ndege zisizo na rubani (drones) dhidi ya meli za kivita za Marekani, ikiwa ni pamoja na manowari ya kubeba ndege ya USS Harry S. Truman, zilizoko Bahari Nyekundu.
Msemaji huyo wa Wahouthi alionya kuwa wataendelea kuzuia usafiri wa meli zinazohusika na Israel katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia hadi Israel itakapositisha uvamizi wake katika Ukanda wa Gaza na kuondoa mzingiro dhidi ya maeneo ya Palestina.
Kwa upande wake, jeshi la Israel limethibitisha kuwa limedungua makombora ya balistiki yaliyorushwa na Wahouthi kwa kutumia mifumo yake ya kujikinga na mashambulizi ya anga.
Mashuhuda waliripoti kusikia milipuko kadhaa huko Jerusalem. Polisi walisema kuwa ving'ora vya hatari vilisikika huko Tel Aviv, Jerusalem, na katika makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi.
Jeshi la Israel liliongeza kuwa limedungua makombora yote mawili ya balistiki kabla hayajaingia katika anga ya Israel.
Wakati huohuo, kituo cha televisheni cha Al-Masirah kinachoendeshwa na Wahouthi kimeripoti kuwa mashambulizi ya anga mfululizo yaliyofanywa na Marekani dhidi ya mji mkuu Sanaa na maeneo ya jirani yamesababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine wawili.