Vita vinavyoendelea nchini Sudan vinazidi kuleta maafa makubwa ya kibinadamu. Mji wa Al-Fashir, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, unakabiliwa na mazingira ya kutisha baada ya kuzingirwa na waasi, hali inayowaweka maelfu ya familia katika hatari ya kufa kwa njaa. Hili ni onyo zito ambalo limetolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Eric Pordyson, ambaye ni Mkuu wa WFP katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, alisema kuwa miaka miwili ya vita imefifisha kabisa mifumo ya kukabiliana na njaa katika mji huo. Aliongeza kuwa, bila msaada wa haraka na endelevu, maisha mengi yatapotea. Hii ni ishara tosha kwamba mzozo wa Sudan unahitaji suluhisho la haraka ili kuepusha maafa ya kibinadamu yanayotishia maisha ya mamilioni ya watu.
Ripoti kutoka Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa takriban asilimia 40 ya watoto walio chini ya miaka mitano huko Al-Fashir wanateseka na utapiamlo mkali, huku asilimia 11 ya watoto hao wakiwa katika hali mbaya. Hili linatokana na ukweli kwamba tangu Mei mwaka jana, Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), ambacho ni kikundi cha waasi, kimeuzingira mji wa Al-Fashir na kufunga barabara zote kuu zinazoingia na kutoka katika mji huo.
Kuzingirwa huku kumesababisha upungufu mkubwa wa chakula kwa mamia ya maelfu ya wakazi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa misaada ya kibinadamu kuwafikia wahitaji. Tangu RSF walipopoteza mji mkuu wa Khartoum mwezi Machi, wameongeza mashambulizi yao katika maeneo ya Al-Fashir na viunga vyake, hali iliyosababisha maelfu ya watu kukimbilia usalama ndani ya mji huo baada ya kambi ya wakimbizi ya Zamzam kushambuliwa mwezi Aprili.
Sudan imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kwa zaidi ya miezi 27 kati ya Jeshi la Serikali na RSF. Ingawa RSF inadhibiti sehemu kubwa ya Darfur Magharibi na Kusini, hivi karibuni walipoteza udhibiti wa Khartoum kwa Jeshi la Serikali, na hivyo sasa pande hizo mbili zinatofautiana kimamlaka. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 20,000 wamepoteza maisha na zaidi ya milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku takriban milioni 4 wakitafuta hifadhi katika nchi jirani kama Chad, Misri, na Sudan Kusini.