Pakistan imejikuta tena katika wimbi la maafa ya mafuriko, huku mamia ya watu wakipoteza maisha kaskazini magharibi mwa nchi. Hali hii imepelekea mamlaka kutoa tahadhari mpya ya mafuriko katika maeneo ya kusini, ikiwa ni miaka miwili tu tangu nchi hiyo ikumbwe na janga kubwa la mafuriko lilosababisha maelfu ya vifo mwaka 2022.
Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Maafa (NDMA), baadhi ya mikoa ya kusini, ikiwemo Karachi, Hyderabad, Thatta, Badin, Mirpurkhas, na Sukkur, inatarajiwa kupokea mvua kubwa inayoweza kufikia milimita 100 ndani ya saa 24 zijazo. Utabiri huu umetolewa huku mamlaka ikionya kuwa barabara kuu zinaweza kuzama, na kusababisha usumbufu mkubwa wa usafiri, pamoja na uharibifu wa miundombinu ya umeme na mawasiliano. Taarifa ya NDMA inaeleza kuwa tayari mvua zilizonyesha katika masaa 24 yaliyopita zimesababisha vifo vya watu 41 nchini kote, wengi wao wakiwa kutoka mkoa wa Gilgit-Baltistan kaskazini na mji wa Karachi. Shule nyingi jijini Karachi zimefungwa kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa siku moja kabla.
Tangu Juni 26, mvua za masika zisizo za kawaida zimechangia vifo vya jumla ya watu 746 nchini Pakistan. Katika mkoa wa Buner, kaskazini magharibi, timu za uokoaji zinaendelea na kazi ngumu ya kutafuta takriban watu 150 waliopotea baada ya mafuriko, yaliyobeba mawe na tope, kuharibu kabisa vijiji na kuacha nyumba zikiwa magofu. Kazi hii ya uokoaji, inayohusisha pia mbwa maalumu wa jeshi, inafanyika mbele ya macho ya jamaa wenye hofu, huku miili zaidi ikifukuliwa kutoka kwenye vifusi. Msemaji wa huduma za uokoaji, Mohammad Sohail, amethibitisha kuwa idadi ya vifo katika eneo la Buner imeongezeka hadi 290. Timu hizo zimekuwa zikitoa msaada wa mahema, mablanketi, vifaa vya kupikia, chakula cha dharura, na maji safi ya kunywa kwa waathirika.
Waziri Mkuu Shehbaz Sharif na Mkuu wa Jeshi Asim Munir walitembelea maeneo yaliyoathirika vibaya ya Bonde la Swat na Buner, kujionea wenyewe athari za mafuriko. Pamoja na juhudi za serikali, baadhi ya wakazi wameonyesha kukerwa, wakilalamika kuwa hawakupewa tahadhari za mapema za kutosha kutoka kwa serikali. Hali hii inazua maswali mengi kuhusu utayari wa nchi kukabiliana na majanga haya yanayojirudia, hasa katika mazingira ya mabadiliko ya tabianchi.