Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, bado yupo chini ya uangalizi wa kitabibu baada ya kugundulika kuwa na tatizo la figo. Hata hivyo, Vatican imeripoti kuwa hali yake inaimarika na hakuna dalili mpya za matatizo ya kupumua.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Vatican ilieleza kuwa Papa Francis anaendelea kutumia oksijeni yenye mtiririko mkubwa na alikuwa amepewa damu. Vipimo vya kitabibu vinaonyesha kuwa ana tatizo dogo la figo, lakini hali hiyo kwa sasa inadhibitiwa na madaktari.
Licha ya changamoto za kiafya, Vatican imebainisha kuwa Papa Francis anaendelea kuwa mwenye ufahamu mzuri na anaweza kujieleza.
Papa Francis alilazwa katika Hospitali ya Gemelli jijini Roma, Italia, mnamo Februari 14 baada ya kupata shida za kupumua kwa siku kadhaa. Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina, madaktari waligundua kuwa alikuwa na homa ya mapafu iliyoshambulia mapafu yote mawili.
Jumapili asubuhi, licha ya hali yake ya kiafya, Papa aliweza kushiriki Misa Takatifu akiwa hospitalini pamoja na wahudumu wanaomhudumia.
Taarifa hii mpya inakuja siku moja baada ya Vatican kueleza kuwa hali ya Papa ilikuwa "mbaya sana" kutokana na tatizo la kupumua. Jumapili hiyo hiyo, Papa Francis alitoa ujumbe akiomba waumini waendelee kumuombea, baada ya kushindwa kuhudhuria ibada ya jadi ya kila Jumapili kwa wiki ya pili mfululizo.
Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, amekuwa akihitaji huduma za kitabibu mara kwa mara katika miaka yake 12 ya uongozi wa Kanisa Katoliki. Mwaka 2023, alipata matibabu ya dharura kwa sababu za kiafya.
Akitokea Argentina, Papa Francis ni Kiongozi wa Kwanza wa Kanisa Katoliki kutoka bara la Amerika Kusini na wa kwanza kutoka shirika la Jesuit.