Utalii wa Ngono Washamiri Japani: Waziri Mkuu Takaichi Aapa Kutokomeza 'Aibu ya Taifa'

international | Sun Nov 09 2025


Utalii wa Ngono Washamiri Japani: Waziri Mkuu Takaichi Aapa Kutokomeza 'Aibu ya Taifa'

Serikali ya Japani imekabiliwa na shinikizo kali la ndani na kimataifa kufuatia kuibuka kwa taarifa za kuongezeka kwa biashara ya ukahaba inayofanywa na wanawake wa Kijapani, ikiwalenga moja kwa moja watalii wa kigeni. Hali hii imeibua mjadala mkali bungeni, na kumlazimu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bi. Sanae Takaichi, kutoa ahadi nzito ya kulishughulikia suala hilo.


Katika kikao cha Baraza la Juu la Bunge (sawa na Seneti) kilichofanyika Novemba 6, kiongozi huyo wa Japani alibanwa vikali na maswali kutoka kwa wabunge wa upinzani kuhusu jambo hilo linalochafulia sifa ya taifa hilo la Asia.


Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu Takaichi alikiri uzito wa suala lenyewe, akisema, "Haya ni maoni mazito sana yanayolenga kulinda utu wa wanawake wetu na heshima ya Japani." Aliahidi bayana kwamba serikali yake "itafanya jitihada za dhati kutokomeza biashara ya ukahaba."


Suala hili liliibuliwa kwa ukali na Mbunge wa upinzani kutoka chama cha Kidemokrasia cha Katiba, Bi. Shiomura Fumika. Bi. Fumika alilieleza bunge kuwa sasa hivi vyombo vya habari vya kimataifa vimeanza kuipa Japani jina jipya la "nchi ya utalii wa ngono."


Alionya kuwa taswira hasi inaenea kimataifa kwamba "Japani ni nchi isiyolinda utu wa wanawake." Bi. Fumika alieleza kwa uchungu jinsi nchi hiyo sasa inavyotazamwa kama "mahali salama kwa wanaume wa kigeni kuja kununua huduma za ngono bila shida."


Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kueleza kuhusu "mfumo potofu" uliopo, ambapo mara nyingi ni wanawake wanaouza miili yao ndio wanaokamatwa na kuadhibiwa na sheria, huku wateja na wawezeshaji wakiachwa. Alisisitiza kuwa hali hii sio tu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wanawake, bali pia inahatarisha sifa ya Japani kimataifa. Alionya kwamba ikiwa nchi itaonekana kama kitovu cha fedha zinazotokana na uhalifu (kama ukahaba), itapoteza kuaminika kwake katika ulingo wa kimataifa.


Katika majibu yake, Waziri Mkuu Takaichi aliahidi kuwa serikali itafanya mapitio ya kina kuhusu kanuni na sheria zinazohusu biashara ya ukahaba, ikizingatia mabadiliko ya sasa ya kijamii.


Aidha, kiongozi huyo aligusia suala la uhalifu uliopangwa. Alisisitiza haja ya kuzuia makundi ya kihalifu yanayofahamika nchini humo kama "Tokuryu" — ambayo ni makundi ya uhalifu yasiyo na kiongozi mmoja maalum au muundo rasmi, na yanayobadilika badilika. Alisema makundi haya yanatumia biashara ya ukahaba kama chanzo kikuu cha mapato yao haramu.


"Tutahakikisha tunatokomeza ukahaba na kuangamiza kabisa makundi haya ya Tokuryu," Waziri Mkuu Takaichi alihitimisha kwa msisitizo.


Wachambuzi wa mambo ya kijamii wanaeleza kuwa ongezeko hili la biashara ya ngono limechochewa na mambo kadhaa. Kwanza ni kufunguliwa kwa mipaka baada ya janga la UVIKO-19, kulikoruhusu watalii wengi kumiminika nchini humo. Hata hivyo, sababu kuu inatajwa kuwa ni hali ngumu ya kiuchumi.


Ripoti za vyombo vya habari vya kigeni zinaeleza kuwa thamani ya fedha ya Japani (Yen) imeporomoka sana, na wakati huo huo kumekuwa na ongezeko la umaskini na watu wenye kipato cha chini. Hali hii inawafanya baadhi ya wanawake wa Kijapani kukosa njia mbadala na kujikuta wakilazimika kuingia kwenye biashara hiyo ili kujikimu, wakilenga watalii kutoka nchi kama China, ambao fedha zao zina nguvu zaidi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.