Uchumi mkubwa zaidi duniani, ule wa Marekani, unakabiliwa na ishara za hatari ambazo hazijashuhudiwa kwa muda mrefu. Ripoti mpya zinaonyesha kuwa idadi ya makampuni makubwa na ya kati yanayotangaza kufilisika na kufunga biashara nchini humo inatazamiwa kufikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Shirika la habari la Reuters, likinukuu takwimu kutoka kwa wachambuzi wa S&P Global, limebainisha kuwa hali hii inaonyesha "msongo" (stress) mkubwa uliokusanyika kwa muda mrefu ndani ya sekta mbalimbali za biashara nchini Marekani.
Takwimu zilizokusanywa tangu mwanzo wa mwaka huu hadi mwezi Oktoba pekee, zinaonyesha kuwa tayari jumla ya maombi 655 ya kufilisika yamepokelewa. Idadi hii ni ya kutisha ikilinganishwa na ukweli kwamba inakaribia kufikia idadi ya mwaka mzima uliopita, ambapo maombi 687 yalirekodiwa. Hii ina maana kuwa kasi ya kufilisika imeongezeka karibu maradufu.
Mwelekeo huu unaonekana kushika kasi zaidi miezi ya hivi karibuni. Mwezi Agosti mwaka huu pekee ulishuhudia maombi 76, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kwa mwezi mmoja tangu ilivyokuwa mwaka 2020. Hali haikutulia, kwani mwezi Oktoba nao ulikuwa na maombi 68, ikiendelea kuonyesha hali mbaya.
Uchambuzi wa kina unaonyesha kuwa sekta ya Viwanda (Industrial) ndiyo imeathirika zaidi, ambapo kampuni 98 zimetangaza kufilisika. Hii inatajwa kuchangiwa na mivutano ya kimataifa ya ugavi (supply chain) pamoja na athari za muda mrefu za ushuru wa forodha. Inayofuata kwa karibu ni sekta ya Bidhaa za Matumizi (Consumer Discretionary), ambapo kampuni 80 zimefunga milango. Hii ni ishara dhahiri kwamba watumiaji wa kawaida, hasa wale wa kipato cha chini, wanakabiliwa na wakati mgumu kifedha.
Chanzo cha Tatizo ni Nini?
Wachambuzi wa Reuters wanaeleza kuwa kuna mchanganyiko wa sababu kadhaa zinazochochea wimbi hili la mafilisi. Kwanza, bado kuna sintofahamu kuhusu athari za mwisho za sera za ushuru wa forodha zilizoanzishwa miaka kadhaa nyuma, ambazo zimeendelea kusababisha kupanda kwa gharama za uendeshaji kwa makampuni mengi.
Pili, tatizo la mfumuko wa bei (inflation) ambao umeshikilia kwa muda mrefu bila kushuka kama ilivyotarajiwa. Tatu, soko la ajira linaloanza kuonyesha dalili za kudhoofika. Hali hii inawaumiza zaidi watumiaji wa kipato cha chini, na hivyo kupunguza uwezo wao wa kununua bidhaa na huduma.
Hata hivyo, ripoti ya S&P inaweka wazi kuwa mzizi mkuu wa tatizo hili ni hatua za Benki Kuu ya Marekani (The Fed). Mwelekeo huu wa filisi umeanza kushika kasi tangu mwaka 2022, pale ambapo Benki Kuu hiyo ilipoanza kupandisha viwango vya riba kwa kasi ya ajabu ili kujaribu kupambana na mfumuko wa bei. Ingawa lengo lilikuwa jema, hatua hiyo imefanya gharama za mikopo kuwa ghali mno. Makampuni yaliyokuwa yamejiendesha kwa kutegemea mikopo sasa yanajikuta yameshindwa kulipa madeni hayo, na hivyo kulazimika kufunga biashara.
Hofu Yatanda Kwenye Masoko ya Mikopo
Hali hii imeanza kuwatia hofu wawekezaji wakubwa na mabenki (Wall Street) kuhusu afya ya soko zima la mikopo. Hivi karibuni, kampuni kubwa ya vifaa vya magari ya FirstBrands ilitangaza kufilisika kutokana na mzigo usiabebeka wa madeni.
Mbaya zaidi, siku chache baadaye, kampuni mbili za fedha zilizokuwa zikitoa mikopo ya magari kwa watu wenye historia mbaya ya mikopo (subprime), zinazojulikana kama Tricolor na PrimaLend Capital, nazo zikafuata mkondo.
Kufilisika kwa kampuni hizi kumesababisha hasara ya moja kwa moja kwa mabenki makubwa. Benki kubwa zaidi nchini Marekani, JP Morgan Chase, imethibitisha kulazimika kufuta deni la Dola za Kimarekani milioni 170 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 442) ambayo ilikuwa imeikopesha kampuni ya Tricolor. Hii ni ishara tosha kwamba tatizo linaanza kuenea na kugusa taasisi kubwa za fedha.