Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza mpango wa kununua na kumiliki Ukanda wa Gaza, hatua iliyozua upinzani mkubwa duniani. Trump alieleza kuwa lengo la pendekezo hilo ni kuhamisha Wapalestina wapatao milioni mbili kutoka Gaza na kuboresha maisha yao kwa msaada wa mataifa ya Kiarabu.
Akizungumza na wanahabari, Trump alisema kuwa ana mpango wa kushirikiana na mataifa ya Kiarabu kukarabati miundombinu katika maeneo yatakayowapokea Wapalestina walioko Gaza. Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha raia wa Palestina wanaishi maisha mazuri na salama.
Hata hivyo, Mamlaka ya Palestina na kundi la Hamas, ambalo limekuwa likipigana na Israel kwa zaidi ya miezi 16, walikataa vikali pendekezo hilo. Mamlaka ya Palestina ilisema, "Ardhi ya Palestina sio ya kuuzwa."
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisifu pendekezo la Trump, akilitaja kuwa "mwamko mpya na bunifu" wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa mzozo wa Gaza.
Pendekezo hili la Trump linakuja wiki tatu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika Gaza kuanza kutekelezwa. Katika makubaliano hayo, Hamas iliwaachilia huru baadhi ya mateka wa Israel waliokuwa wakizuiliwa, kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko magerezani Israel.
Hali ya mzozo Gaza imezidi kuwa mbaya tangu Oktoba 7, 2023, wakati wanajeshi wa Israel walipoanzisha operesheni kubwa baada ya shambulizi la kushtukiza lililosababisha vifo vya watu 1,200 na mateka 251 kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas, zaidi ya watu 48,180 wameuawa Gaza tangu mapigano hayo kuanza, huku maelfu wakijeruhiwa na wengine kupoteza makazi yao.
Mpango wa Trump umeibua mijadala mikali na maswali kuhusu mustakabali wa Wapalestina na athari za hatua hiyo kwa mchakato wa amani katika ukanda huo.