Katika kile kinachoonekana kama mtikisiko mkubwa zaidi wa kijeshi kuwahi kutokea nchini Marekani katika miongo ya hivi karibuni, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) ipo mbioni kufanya mabadiliko makubwa ya kimuundo ambayo yataigusa moja kwa moja Bara la Afrika.
Taarifa nyeti zilizovuja kupitia gazeti lenye ushawishi mkubwa la *Washington Post (WP)*, zinaeleza kuwa utawala wa Rais Donald Trump unakusudia "kufumua" mfumo wa sasa wa amri za kijeshi duniani, kwa lengo la kupunguza nguvu ya Marekani nje ya mipaka yake na kuelekeza nguvu zaidi kulinda nyumbani, ikiwa ni utekelezaji wa sera yake maarufu ya "Marekani Kwanza" (America First).
Afrika, Ulaya na Mashariki ya Kati: Kapu Moja
Kwa mujibu wa mpango huo, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Cain, anatarajiwa kuwasilisha pendekezo kwa Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, la kupunguza idadi ya Kamandi za Kivita (Combat Commands) kutoka 11 hadi kubaki 8 tu.
Kwenye mabadiliko hayo, Kamandi ya Marekani kwa ajili ya Afrika (AFRICOM), ambayo imekuwa ikishirikiana na nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania katika masuala ya ulinzi na kupambana na ugaidi, inatarajiwa kuunganishwa na Kamandi ya Ulaya (EUCOM) pamoja na ile ya Mashariki ya Kati (CENTCOM). Muungano huu utaunda kamandi mpya itakayoitwa "International Command" (Kamandi ya Kimataifa).
Hii inatafsiriwa kama kushushwa kwa hadhi ya maeneo hayo katika vipaumbele vya kijeshi vya Marekani, huku wachambuzi wakidai kuwa hatua hii inalenga kupunguza gharama na idadi ya Majenerali wa Nyota Nne (4-Star Generals) ambao wamekuwa wengi.
Kuzaliwa kwa 'Americom'
Wakati Afrika na Ulaya zikiwekwa kapu moja, Marekani inajipanga kuimarisha ulinzi wa nyumbani. Mpango huo unapendekeza kuunganishwa kwa Kamandi ya Kaskazini (inayolinda Marekani na Canada) na Kamandi ya Kusini (inayolinda Amerika ya Kusini na Karibiani) ili kuunda chombo kipya kitakachoitwa "Americom" au "Kamandi ya Amerika".
Lengo kuu ni kuhamishia rasilimali za kijeshi kutoka mataifa ya mbali na kuzileta karibu na nyumbani ili kulinda "Bara la Amerika" dhidi ya matishio ya kiusalama, wahamiaji haramu na dawa za kulevya, jambo ambalo linaendana na falsafa ya Trump inayosema, "Zama za Marekani kuwa kama Atlas anayebeba dunia mabegani mwake zimepita."
China Bado ni Tishio
Licha ya mabadiliko hayo makubwa, eneo moja ambalo halitaguswa ni Kamandi ya Indo-Pasifiki (Indo-Pacific Command). Eneo hili linalosimamia mikakati ya Marekani dhidi ya China, Korea Kaskazini na ulinzi wa Taiwan litaendelea kubaki kama lilivyo.
Hii inaashiria kuwa, licha ya Trump kutaka kujikita nyumbani, bado anaichukulia China kama tishio namba moja kwa usalama wa Marekani na uchumi wake, hivyo hataki kulegeza kamba katika eneo hilo la kimkakati linalohusisha ukanda wa "First Island Chain" (Mlolongo wa Visiwa vya Kwanza).
Bunge la Marekani Laita 'Stop'
Hata hivyo, mpango huu huenda ukakumbana na kigingi kigumu kutoka kwa Bunge la Marekani (Congress). Wabunge wameanza kuonesha wasiwasi kuwa kuunganisha kamandi hizi kiholela kunaweza kusababisha "Ombwe la Usalama" (Security Vacuum), hasa katika maeneo yenye migogoro kama Mashariki ya Kati na Afrika ambako makundi ya kigaidi bado ni tishio.
Wakati dunia ikisubiri kuona kama Jenerali Cain atafanikiwa kupitisha mpango huu, ni dhahiri kuwa Marekani inataka kubadili jukumu lake la kuwa "Polisi wa Dunia" na kuanza kujijali yenyewe kwanza.