Trump Achokoza Marekani kwa Kofia ya 2028: Anataka Kuvunja Katiba na Kuongoza Muhula wa Tatu?

international | Thu Oct 02 2025


Trump Achokoza Marekani kwa Kofia ya 2028: Anataka Kuvunja Katiba na Kuongoza Muhula wa Tatu?

Kwa mtindo wake wa siasa za vishindo na vituko, Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa mara nyingine amezua mjadala mzito na kuzitikisa siasa za nchi hiyo baada ya kuchapisha picha inayoashiria nia yake ya kuwania urais kwa muhula wa tatu mwaka 2028. Katiba ya Marekani, kupitia Marekebisho ya 22, inazuia waziwazi rais yeyote kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili, hivyo kitendo hiki kimeibua maswali mengi kuhusu nia yake halisi.


Katika picha aliyoiweka kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump anaonekana akiwa katika mkutano mzito na viongozi wa bunge kujadili jinsi ya kuepusha serikali kufungwa (shutdown), lakini juu ya meza yake, kumeonekana kofia nyekundu yenye maandishi "TRUMP 2028". Kofia hiyo ilionekana katika picha zote tatu alizochapisha, ikionyesha kuwa haikuwa bahati mbaya, bali ni ujumbe uliokusudiwa.


Vyombo vya habari nchini Marekani vimepokea kitendo hicho kwa hisia tofauti. Gazeti la New York Post kilikiita ni "kitendo cha dharau kwa mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea," huku kituo cha CNN kikisema ni "ujumbe wa wazi kwa chama cha Democratic." CNN ilimnukuu kiongozi wa Democratic bungeni, Hakeem Jeffries, akisema alimuuliza Makamu wa Rais, J.D. Vance, kuhusu kofia hiyo, lakini Vance alijibu "sina la kusema."


Hii si mara ya kwanza kwa Trump kudokeza kuhusu uwezekano wa kugombea muhula wa tatu. Katika mahojiano na kituo cha NBC mwezi Machi mwaka huu, alisema wazo la kugombea tena "sio utani." Vilevile, katika hotuba yake mjini Las Vegas, alisema itakuwa heshima kubwa "kutumikia si mara moja, mbili, bali tatu au nne."


Ingawa kikatiba safari yake ya muhula wa tatu ni ngumu kwa kuwa inahitaji mabadiliko ya katiba, jambo ambalo haliwezekani bila auni ya wapinzani wake, tayari mbinu mbadala zimeanza kujadiliwa. Moja ya mbinu hizo ni Makamu wake, J.D. Vance, kugombea urais mwaka 2028 huku Trump akigombea umakamu wa rais. Ikiwa watashinda, Vance anaweza kujiuzulu na kumpisha Trump kuchukua urais moja kwa moja. Alipoulizwa kuhusu mbinu hii na NBC, Trump alijibu, "Hiyo ni njia mojawapo. Kuna njia nyingine pia."

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.