Shirika la Hali ya Hewa la Japan (JMA) limetangaza kuwa tetemeko la ardhi lenye ukubwa (magnitude) wa 5.5 lilipiga eneo la Visiwa vya Tokara, Mkoa wa Kagoshima, Kusini mwa Kyushu, Japan, mnamo saa 9:26 alasiri kwa saa za huko, tarehe 2 Julai. Tetemeko hili linakuja kufuatia mfululizo wa matetemeko madogomadogo yaliyoanza tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.
JMA ilithibitisha kuwa hakuna tishio la tsunami kutokana na tetemeko hili, na kwamba kina cha tetemeko kilikuwa kilomita 10. Baadhi ya visiwa vilikumbwa na mitikisiko ya kiwango cha 5-chini (intensity 5-lower). Ni muhimu kufahamu kuwa 'intensity' (kiwango) kinatofautiana na 'magnitude' (ukubwa). Wakati ukubwa unapima nguvu kamili ya tetemeko, kiwango hupima hisia za watu na uharibifu wa vitu katika eneo husika wakati wa tetemeko. Kiwango cha 5-chini kinamaanisha kuwa watu wengi walihisi hofu, na vyombo vya jikoni au vitabu vilivyo juu ya rafu vilianguka.
Visiwa vya Tokara vimekuwa vikishuhudia matetemeko mengi ya ukubwa wa 5 na zaidi, yalianza kupiga mnamo saa 10:30 asubuhi kwa saa za huko, tarehe hiyo hiyo. Gazeti la Yomiuri Shimbun liliripoti kuwa kuanzia tarehe 21 Juni hadi saa 4:00 asubuhi ya tarehe 2 Julai, jumla ya matetemeko 877 yenye kiwango cha 1 au zaidi yalitokea katika eneo hilo.
Mfululizo huu wa matetemeko madogomadogo kwa zaidi ya siku kumi umesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi. Afisa mmoja kutoka Kijiji cha Toshima aliliambia Yomiuri kwamba “wazee wengi wanalalamika uchovu kutokana na matetemeko ya muda mrefu,” na kuongeza kuwa “wanahitaji uangalizi wa kimwili na kiakili.”
JMA imetoa onyo, ikisema kuwa “shughuli za tetemeko la ardhi zinaendelea kwa kasi sana.” Imewataka wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na mitikisiko mikali kuwa makini na matetemeko yenye kiwango cha 5-chini kwa muda usiojulikana. Visiwa vya Tokara viliwahi kukumbwa na matetemeko madogomadogo zaidi ya 300 mfululizo mwezi Desemba 2021 na Septemba 2023.