Dar es Salaam inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tukio la kihistoria wakati Rais Samia Suluhu Hassan atapokea idadi kubwa ya viongozi wakuu wa nchi, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania. Viongozi hao, wakiwemo Wakuu wa Nchi 25, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, na Naibu Mawaziri Wakuu 10, watashiriki Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema tukio hili litaweka rekodi ya kuwa mkutano wenye idadi kubwa zaidi ya viongozi wakuu wa nchi kuwahi kufanyika nchini Tanzania.
“Tanzania iliwahi kupokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1999, na Wakuu wa Nchi 15 walihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019. Hata hivyo, idadi ya viongozi watakaoshiriki mkutano huu wa nishati ni kubwa zaidi,” alisema Balozi Kombo.
Alizitaja nchi ambazo viongozi wao wamethibitisha kushiriki kuwa ni Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guinea-Bissau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti, na Gabon.
Makamu wa Rais watakaoshiriki wanatoka Gambia na Benin, huku Mawaziri Wakuu wakitoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe, na Equatorial Guinea, na Naibu Mawaziri Wakuu kutoka Eswatini na Namibia.
Tanzania Kunufaika na Diplomasia ya Nishati
Balozi Kombo alisema mkutano huo ni moja ya matunda ya diplomasia inayozidi kuimarika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Alieleza kuwa juhudi za Tanzania kujitangaza kimataifa zinaendelea kuzaa matunda, hasa baada ya mwaliko wa Rais Samia kushiriki Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil Novemba 2024.
Aidha, nafasi aliyopewa Rais Samia ya kuzungumza kwa niaba ya Afrika katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) ni ishara ya kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika medani za kimataifa.
Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuharakisha upatikanaji wa nishati safi, nafuu, na endelevu kwa bara la Afrika, huku ukiweka Tanzania katika nafasi muhimu ya kiuchumi na kidiplomasia barani Afrika na duniani.