Taharuki Ulaya: Urusi Inaweza Kuishambulia NATO Hata Kesho, Jemedari Mkuu Ujerumani Aonya

international | Sat Nov 08 2025


Taharuki Ulaya: Urusi Inaweza Kuishambulia NATO Hata Kesho, Jemedari Mkuu Ujerumani Aonya

Wakati vita nchini Ukraine vikiingia mwaka wake wa nne, hali ya wasiwasi barani Ulaya imechukua sura mpya kufuatia kauli nzito iliyotolewa na mmoja wa viongozi wakuu wa jeshi la Ujerumani. Onyo hili linakuja wakati ambapo mataifa ya Magharibi yanaendelea kupima uwezo na nia ya Urusi baada ya miaka kadhaa ya mapigano makali.


Jemedari Alexander Sollfrank, ambaye ni Kamanda wa Operesheni za Jeshi la Shirikisho la Ujerumani, ametoa kauli ya kutisha akisema kuwa Urusi ina uwezo wa kijeshi wa kuanzisha mashambulizi dhidi ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) wakati wowote, hata kesho. Akizungumza na shirika la habari la Reuters mnamo tarehe 7 Novemba, Jemedari Sollfrank alifafanua kuwa shambulio hilo linaweza kuwa la "kiwango kidogo" na la "muda mfupi" kutokana na ukweli kwamba Urusi bado imejikita zaidi kwenye vita vyake nchini Ukraine.


Licha ya uwezekano huu wa shambulio la ghafla, Jemedari huyo pia alirejelea makadirio mengine ya maafisa wa usalama barani Ulaya ambayo yanazungumziwa sana kwa sasa. Makadirio hayo yanaonya juu ya uwezekano wa Urusi kuanzisha uvamizi mkubwa na wa kina dhidi ya NATO ifikapo mwaka 2029.


Huu ni mabadiliko makubwa katika mtazamo wa usalama wa Ulaya. Hapo awali, wakati vita vya Ukraine vilipoanza, wachambuzi wengi wa Magharibi waliamini kuwa Urusi ingehitaji takriban miaka kumi (10) ili kujijenga upya kijeshi kabla ya kuwa tishio la moja kwa moja kwa NATO. Hata hivyo, sasa inaonekana makadirio hayo yamepunguzwa kwa kasi, huku wengi wakiamini tishio hilo linaweza kuwa halisi ndani ya miaka mitatu (3) hadi mitano (5) ijayo.


Akifafanua msingi wa tathmini yake, Jemedari Sollfrank alichambua hali ya jeshi la Urusi. Alisema kuwa, "Jeshi la Anga la Urusi bado lina nguvu kubwa ya kivita." Aliongeza kuwa vikosi vya nyuklia na makombora ya Urusi havijaathiriwa kabisa na vita vya Ukraine. "Ni kweli kwamba Meli za Kivita za Bahari Nyeusi (Black Sea Fleet) zimepata hasara kubwa, lakini meli nyingine za jeshi la wanamaji la Urusi hazijapata hasara yoyote," alieleza Jemedari Sollfrank.


Alimalizia kwa kusema kuwa uamuzi wa Urusi kushambulia NATO utategemea mambo matatu makuu: uwezo wa kijeshi uliobaki, mafanikio ya kijeshi (ikiwemo Ukraine), na maamuzi ya viongozi wake wa juu. "Kwa kuzingatia mambo haya matatu, tumefikia hitimisho kwamba shambulio la Urusi liko ndani ya wigo wa uwezekano," alisisitiza.


Jemedari Sollfrank, ambaye ana cheo cha Luteni Jenerali, anachukuliwa kuwa mtaalamu wa masuala haya. Kabla ya kushika wadhifa wake wa sasa wa kusimamia operesheni zote za ndani na nje za jeshi la Ujerumani Oktoba mwaka jana, alihudumu kama Kamanda wa Usafirishaji na Vifaa wa NATO. Mwaka jana pia, aliandika tasnifu yake ya uzamivu (PhD) kuhusu mazingira ya kinadharia ya uvamizi wa Urusi dhidi ya nchi za Baltic (Latvia, Lithuania, na Estonia).

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.