Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuhusu uvujaji wa taarifa nyeti uliofanyika baada ya maafisa waandamizi wa usalama wa taifa wa Marekani kumualika kwa bahati mbaya mwandishi wa habari kwenye mazungumzo ya mtandaoni yaliyokuwa yakijadili mipango ya mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, ambao wana uhusiano na Iran.
Mhariri wa jarida la The Atlantic, Jeffrey Goldberg, alifichua mnamo Machi 24 kwamba alijikuta ameongezwa kwenye gumzo la kikundi la viongozi wa usalama wa taifa walipokuwa wakijadili kuhusu mashambulizi hayo ya Yemen. Ikulu ya White House ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Katika ripoti yake, Goldberg alisema kuwa dunia ilikuja kujua kuhusu mashambulizi ya Marekani dhidi ya malengo ya Houthi kote Yemen mnamo Machi 15, saa 2:00 usiku kwa saa za Marekani Mashariki. Hata hivyo, yeye alifahamu kuhusu operesheni hiyo masaa mawili kabla ya bomu la kwanza kulipuka.
Alieleza kuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, alimwongeza kimakosa kwenye programu ya ujumbe mfupi ya kibiashara iitwayo 'Signal'. Kupitia gumzo hilo, saa 11:44 asubuhi ya Machi 15, alipokea 'mpango wa vita' kutoka kwa Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth.
Goldberg aliongeza kuwa mpango huo ulijumuisha taarifa kuhusu aina ya silaha zitakazotumika, malengo yaliyokusudiwa, na muda wa operesheni.
Jarida la Wall Street liliripoti kuwa gumzo hilo lilihusisha watumiaji 18, wakiwemo Makamu wa Rais J.D. Vance, na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio.
Vyombo vya habari kama vile New York Times vimeeleza kuwa tukio hilo ni tatizo sio tu kwa sababu taarifa zilishirikishwa kimakosa na vyombo vya habari, bali pia kwa sababu taarifa nyeti sana zilijadiliwa kupitia programu ya ujumbe isiyo rasmi.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alipoulizwa kuhusu suala hilo katika hafla ya kutangaza uwekezaji wa kampuni ya Hyundai Motor Group nchini Marekani, alisema "sijui chochote" na alipuuza jarida la The Atlantic akisema ni "jarida linalokufa hivi karibuni" na "sifikirii kama ni jarida."
Baadaye, Ikulu ya White House ilitoa taarifa kupitia msemaji wake ikisema kuwa mashambulizi dhidi ya Houthi yalifanikiwa sana na kwamba Rais Trump ana imani kubwa na mshauri wake Waltz pamoja na timu yake ya usalama wa taifa.