Kumeibuka sintofahamu kubwa katika siasa za kimataifa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kujitenga hadharani na shambulio la anga lililofanywa na Israel dhidi ya viongozi wa Hamas katika mji mkuu wa Qatar, Doha. Trump, kupitia mtandao wa Truth Social, alisisitiza kuwa uamuzi huo mzito ulikuwa wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pekee, na haukubarikiwa na serikali yake.
Katika taarifa yake iliyoonesha kutofurahishwa, Trump alisema, "Asubuhi ya leo, tulipokea taarifa za kusikitisha kwamba Israel inashambulia Hamas ndani ya Doha. Huu ni uamuzi wa Waziri Mkuu Netanyahu, sio wangu." Aliongeza kuwa kitendo cha kuishambulia Qatar, nchi huru, mshirika muhimu wa Marekani na ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa bidii na kujitolea katika harakati za upatanishi wa amani, hakitumikii maslahi ya Israel wala Marekani.
Hata hivyo, Trump alibainisha kuwa lengo la kuwaondoa viongozi wa Hamas, ambao alisema "wananufaika na mateso ya watu wa Gaza," ni jambo lenye thamani. Msimamo huu unaonesha jinsi Marekani inavyojaribu kutembea katika mstari mwembamba wa kidiplomasia: kuiunga mkono Israel katika lengo lake la kuisambaratisha Hamas, huku ikijaribu kutuliza hasira za Qatar, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu katika mzozo huo.
Trump alifichua kuwa alimwagiza mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, aitaarifu Qatar kuhusu shambulio hilo lililokuwa karibu kutokea, lakini kwa bahati mbaya, "ilikuwa ni kuchelewa mno kusitisha shambulio hilo." Alielezea masikitiko yake makubwa kuhusu eneo la shambulio, akisisitiza hadhi ya Qatar kama rafiki na mshirika.
Katika juhudi za kuzima moto wa kidiplomasia, Trump alithibitisha kuwa alizungumza kwa simu na Netanyahu mara tu baada ya shambulio na kupata hakikisho la nia ya Israel ya kutafuta amani haraka. Pia, alizungumza na Amiri pamoja na Waziri Mkuu wa Qatar, akiwashukuru kwa urafiki wao na kuwaahidi kuwa "kitendo kama hiki hakitatokea tena katika ardhi yao."
Ili kuimarisha uhakikisho huo, Trump alitangaza kuwa amemuelekeza Waziri wake wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, kuharakisha na kukamilisha makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi na Qatar. Wakati huohuo, Ikulu ya White House ilitoa taarifa inayofanana na msimamo wa Rais.
Shambulio hili la Israel, ambalo limeripotiwa kuhusisha zaidi ya ndege 10 za kivita, limeilenga ofisi ya kisiasa ya Hamas iliyoko Doha. Qatar, ambayo imekuwa mwenyeji wa mazungumzo mengi ya kusitisha mapigano, imesema haikupokea taarifa yoyote ya awali kuhusu shambulio hilo, huku Israel ikidai kuwa mpango huo umekuwa ukiandaliwa kwa wiki kadhaa. Wakati Netanyahu akiona shambulio hili kama "fursa ya kumaliza vita," upande wa Qatar unaliona kama dharau na kitendo kinachodhoofisha mchakato mzima wa amani.