Habari za kushtusha kutoka shirika la habari la Reuters zinafichua kuwa kiasi kikubwa cha chakula cha msaada, ambacho kilipaswa kuwafikia mamilioni ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika mataifa mbalimbali, sasa kinaozea katika maghala bila matumaini ya kuwafikia walengwa. Hali hii ya kusikitisha inakuja kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kupunguza kwa kiasi kikubwa bajeti ya misaada ya kigeni ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya tarehe 16 Mei, iliyopita, takriban tani 60,000 hadi 66,000 za chakula zimekwama katika maghala yanayosimamiwa na Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu (BHA) chini ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID). Maghala hayo yanapatikana katika maeneo ya Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Djibouti (Afrika Mashariki), na Houston nchini Marekani.
Wafanyakazi wa zamani wa USAID na vyanzo vingine vya ndani vimeeleza kuwa shehena hiyo ya chakula inajumuisha bidhaa muhimu kama vile biskuti za kuongeza nguvu (HEB), mafuta ya kupikia, na nafaka zilizoongezewa virutubishi. Thamani ya chakula hiki inakadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 98, ambazo ni sawa na takriban Shilingi bilioni 253 za Kitanzania. Wataalamu wanakadiria kuwa kiasi hiki cha chakula kingeweza kulisha zaidi ya watu milioni moja kwa kipindi cha miezi mitatu. Kama chakula hiki kingepelekwa kwa wakazi wote wa Ukanda wa Gaza, kingetosha kuwalisha kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu.
Kinachozidisha uzito wa jambo hili ni kwamba sehemu ya chakula hiki inakaribia kumalizika muda wake wa matumizi. Kwa mfano, tani 500 za biskuti za kuongeza nguvu zilizohifadhiwa katika ghala la Dubai, Falme za Kiarabu, zinatarajiwa kumalizika muda wake mwezi Julai mwaka huu wa 2025 na hivyo kulazimika kuteketezwa. Hii ni kinyume kabisa na hali ya kawaida ambapo, kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja wa zamani wa USAID, ni takriban tani 20 tu za chakula ndizo huishia kuharibika kwa mwaka, na mara nyingi kutokana na uharibifu wakati wa usafirishaji au uhifadhi.
Ripoti ya Reuters inaeleza kuwa hata juhudi za kukinusuru chakula hiki kwa kukikabidhi kwa mashirika mengine ya kimataifa ya misaada hazijafanikiwa ipasavyo. Ingawa mapendekezo ya namna hiyo yaliwasilishwa kwa Idara ya Misaada ya Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, idhini ya kutekeleza mpango huo imeendelea kucheleweshwa.
Tatizo hili linatokana na hatua za Rais Trump ambaye, mara tu baada ya kuingia madarakani mwezi Januari mwaka huu, alitangaza mipango ya kupunguza kwa kiasi kikubwa bajeti ya program kuu za misaada ya kigeni za Marekani. Zaidi ya hayo, Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), ambayo inasimamia marekebisho ya muundo wa serikali chini ya utawala wa Trump, imeamua kulivunja kabisa shirika la USAID. Tayari mchakato wa kulisambaratisha shirika hilo unaendelea, na inaripotiwa kuwa wafanyakazi wengi wa USAID wanatarajiwa kupoteza ajira zao katika awamu mbili, Julai 1 na Septemba 2 mwaka huu wa 2025.
Kufuatia kupunguzwa kwa bajeti ya misaada na Marekani, utoaji wa msaada kwa maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, kama vile Ukanda wa Gaza na Sudan, nao umesitishwa. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linakadiria kuwa takriban watu milioni 300 duniani kote wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula unaowatia katika hali ya wasiwasi, huku watu milioni 1.9 wakikabiliwa na njaa kali. Ripoti ya Reuters inabainisha kuwa idadi kubwa ya watu hawa wanapatikana katika Ukanda wa Gaza na Sudan.
Reuters pia imeongeza kuwa kusitishwa kwa misaada ya Marekani kumeathiri pia usambazaji wa chakula maalum cha tiba kwa watoto wenye utapiamlo (RUTF). Jeanette Bailey, Mkurugenzi wa Lishe katika Kamati ya Kimataifa ya Uokozi (IRC), aliliambia shirika la Reuters kuwa ingawa ni vigumu kupima kwa usahihi ukubwa wa athari za kusitishwa kwa bajeti hiyo ya Marekani katika usambazaji wa chakula cha lishe, jambo moja liko wazi: "Kama kituo chochote cha matibabu ya utapiamlo (kituo cha kuleta utulivu) kinachomhudumia mtoto kikikosa kupokea shehena ya matibabu, zaidi ya asilimia 60 ya watoto wenye utapiamlo watakuwa katika hatari kubwa ya kufariki dunia katika siku za karibuni sana."