Hofu na taharuki vimerejea katika jiji la Los Angeles (LA) nchini Marekani, baada ya moto mkubwa wa msitu kutokea na kusambaa kwa kasi, miezi michache tu baada ya eneo hilo kukumbwa na maafa ya moto wa msitu mwingine mapema mwaka huu. Janga hili jipya limeiweka mamlaka ya dharura katika hali ya hatari.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Misitu na Zimamoto ya California, moto huo, unaofahamika kama 'Canyon Fire,' ulianzia majira ya saa saba mchana mnamo Agosti 7, 2025, katika eneo la Castaic, linalounganisha kaunti za Los Angeles na Ventura. Hadi kufikia asubuhi ya leo, moto huo umeteketeza eneo lenye ukubwa wa hekta 7,850, ambalo ni sawa na ukubwa wa takriban mara saba ya eneo la kisiwa cha Mji wa Dar es Salaam. Licha ya jitihada za kuzima moto, mamlaka zinasema hadi sasa hakuna mafanikio yoyote ya kuuzima moto huo.
Zaidi ya maafisa 400 wa zimamoto wametumwa kwenye eneo la tukio kujaribu kudhibiti moto huo mkubwa, ambao bado unaendelea kusambaa kwa kasi. Kutokana na hatari iliyopo, wakazi wapatao 2,500 walioishi katika eneo hilo na karibu na majengo 700 wameamriwa kuondoka mara moja. Wakati huo huo, tahadhari ya kuondoka imetolewa kwa wakazi wengine takribani 14,000 wanaoishi kaskazini mwa Kaunti ya LA. Ingawa ripoti za awali zimeeleza kuwa baadhi ya majengo yameharibika, kiwango kamili cha uharibifu bado hakijajulikana.
Sababu ya moto huu bado inachunguzwa, lakini maafisa wa mamlaka ya dharura wamesema mazingira ya hewa yamechangia pakubwa kuusambaza moto huo. Joto kali la nyuzi joto 37 Celsius na upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa, vimefanya moto kusambaa kwa kasi isiyo ya kawaida. Mtaalamu wa hali ya hewa kutoka Huduma ya Hali ya Hewa ya Kitaifa (NWS), Mike Warford, ametoa tahadhari kuwa hatari ya moto itaendelea wiki nzima kutokana na hali ya hewa yenye joto kali na hewa kavu.
Msimamizi wa Serikali ya Kaunti ya LA, Kathryn Barger, amewasihi wananchi kuzingatia maagizo ya kuondoka mara moja. Alisema kuwa joto na ukavu katika kaunti hiyo vinatengeneza mazingira hatari kwa moto kusambaa haraka, na kuwakumbusha wananchi kuhusu maafa ya 'Eaton Fire' ya mwezi Januari mwaka huu, ambayo yalionyesha jinsi moto unavyoweza kuleta uharibifu mkubwa na wa ghafla. Moto huo ulioteketeza zaidi ya nyumba na majengo 18,000 na kuua watu 29.