Mkurugenzi wa Kipalestina, Hamdan Ballal, ambaye filamu yake ya makala 'No Other Land' ilishinda tuzo ya Oscar hivi karibuni, ameshambuliwa na kundi la walowezi wa Israel katika nyumba yake iliyoko Ukingo wa Magharibi. Baada ya kushambuliwa, alikamatwa na wanajeshi wa Israel.
Taarifa kutoka kwa Youval Abraham, mmoja wa watayarishaji wa filamu hiyo, zinasema kuwa walowezi kadhaa wa Israel walimvamia Ballal na kumsababishia majeraha kichwani na tumboni hadi kuvuja damu. Abraham alieleza kuwa wanajeshi waliingilia gari la wagonjwa ambalo lilikuwa limemchukua Ballal na kumtoa nje, kisha wakampeleka kusikojulikana.
Basel Adra, ambaye alishirikiana na Ballal kuongoza filamu hiyo, alithibitisha kupokea taarifa kuhusu tukio hilo na alipofika eneo la tukio katika kijiji cha Susya, alishuhudia mtu akiburuzwa. Aliongeza kuwa alishuhudia kundi la walowezi wa Israel nje ya nyumba ya Ballal, wengine wakiwa wanarusha mawe. Wanajeshi wa Israel pia walikuwepo na walifyatua risasi ili kuwazuia watu kukaribia.
Jeshi la Israel limesema kuwa linachunguza taarifa hizo.
Filamu ya 'No Other Land' inaelezea maisha ya Wapalestina wanaoishi Ukingo wa Magharibi. Ballal, ambaye ni mkulima, anaelezea katika filamu hiyo jinsi anavyokabiliwa na vitisho vya kupokonywa nyumba na ardhi na walowezi wa Israel.
Katika tukio hilo hilo, wanaharakati watano wa Marekani kutoka shirika lisilo la kiserikali la 'Kituo cha Wayahudi kwa Ajili ya Ukosefu wa Vurugu', ambao wanapinga makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi, pia walishambuliwa na walowezi wa Israel. Shirika hilo lilisema kuwa walowezi kadhaa walishambulia kijiji hicho kwa silaha kama vile marungu na visu, na wengine walifyatua risasi.
Josh Kimmelman, mmoja wa wanaharakati hao, aliiambia CNN kuwa wanajeshi wa Israel walikuwepo lakini hawakufanya chochote kuwazuia walowezi hao.