Ulimwengu wa sanaa nchini Hispania umetawaliwa na sintofahamu baada ya mchoro mdogo lakini wenye thamani kubwa wa mchoraji mashuhuri duniani, Pablo Picasso, kuripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha wakati ukiwa unasafirishwa kwenda kwenye maonyesho.
Polisi nchini humo wameanzisha uchunguzi wa kina kufuatilia kutoweka kwa kazi hiyo ya mwaka 1919, inayojulikana kama 'Still Life with Guitar' (Taswira Tuli na Gitaa). Thamani ya mchoro huo inakadiriwa kufikia Euro 600,000, kiasi ambacho ni sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 1.7.
Mchoro wenyewe ni mdogo sana, ukiwa na ukubwa wa sentimita 12.7 kwa sentimita 9.8 tu, na ulichorwa kwa kutumia rangi za guoashi (gouache) na penseli. Hii ni moja ya kazi zilizokuwa zikisafirishwa kutoka kwa mkusanyaji binafsi jijini Madrid kwenda kusini mwa nchi hiyo, katika jiji la Granada, kwa ajili ya maonyesho mapya yaliyoandaliwa na Taasisi ya CajaGranada.
Mkasa huu ulianza tarehe 3 mwezi huu, wakati kundi la kazi za sanaa za mkopo, ikiwemo hiyo ya Picasso, liliposafirishwa kwa gari. Mizigo hiyo iliwasili kwenye jumba la maonyesho majira ya saa nne asubuhi na taratibu za upakuaji na ukaguzi zikaanza.
Hata hivyo, Taasisi ya CajaGranada imetoa maelezo yanayoacha maswali mengi. Walikiri kwamba ingawa upakuaji ulifanyika, "haikuwezekana kukagua baadhi ya kazi" zilizowasili. Licha ya kasoro hiyo kubwa ya kiusalama, waratibu waliruhusu gari na wafanyakazi wa usafirishaji kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za makabidhiano.
Kazi hizo zilihifadhiwa kwenye chumba chenye ulinzi wa kamera za video (CCTV) kwa kipindi chote cha mwisho wa wiki. Siku ya Jumatatu iliyofuata, wafanyakazi wa taasisi walianza kazi ya kufungua vifurushi. Ilikuwa ni wakati huu, "baada ya ukaguzi kamili kukamilika na wafanyakazi kuanza kuhamishia kazi hizo kwenye maeneo mbalimbali ya maonyesho," ndipo mtunza maonyesho na msimamizi waligundua kuwa mchoro mmoja haukuwepo.
Taasisi hiyo imesisitiza kuwa walitoa taarifa mara moja kwa Polisi ya Kitaifa na wanaendelea kutoa ushirikiano kamili. "Tuna imani kamili kwamba suala hili litapatiwa ufumbuzi unaofaa," ilisema taarifa yao.
Kupotea kwa kazi ya Picasso si jambo jipya; sifa zake na thamani ya juu ya kazi zake vimezifanya kuwa sumaku kwa wezi wa sanaa kwa miongo kadhaa. Matukio ya wizi wa kazi za Picasso yamekuwa yakitikisa dunia mara kwa mara.
Kwa mfano, mnamo Februari 2007, wezi walivamia makazi ya mjukuu wa Picasso huko Paris na kuiba michoro miwili yenye thamani ya jumla ya Euro milioni 50 (zaidi ya TZS Bilioni 140). Mwaka 2009, kitabu cha michoro (sketchbook) chenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 8 (zaidi ya TZS Bilioni 22) kiliibwa kutoka kwenye jumba la makumbusho la Picasso.
Mnamo 1989, mjukuu mwingine wa Picasso, Marina, alipoteza kazi 12 za babu yake zenye thamani ya Pauni milioni 9 (karibu TZS Bilioni 30) baada ya wezi kuvamia jumba lake la kifahari kusini mwa Ufaransa. Tukio kubwa zaidi lilitokea 1976 huko Avignon, Ufaransa, ambapo kazi 118 za Picasso ziliibwa kutoka kwenye makumbusho, likitajwa kuwa tukio kubwa zaidi la wizi wa sanaa katika historia ya Ufaransa.
Hata London haikusalimika, kwani mwaka 1997, jambazi aliyevamia jumba la sanaa mchana kweupe aliiba mchoro wa 'Woman's Head' na kutoroka kwa teksi, ingawa baadaye mchoro huo ulipatikana. Uchunguzi unaendelea kubaini kama mchoro huu wa 'Still Life with Guitar' umeibwa au umepotea kwa uzembe.