Hali ya usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea kuzorota kwa kasi, huku kundi la kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye mafungamano na Dola la Kiislamu (IS), likifanya shambulio lingine la kinyama na kuua takriban raia 19 katika kijiji cha Mukondo.
Tukio hili la umwagaji damu lilitokea Jumapili, Oktoba 12, katika eneo la Lubero, Mkoa wa Kivu Kaskazini. Kwa mujibu wa mkuu wa kijeshi wa eneo hilo, Alain Kiwewa, wanamgambo wa ADF walivamia kijiji hicho usiku, wakachinja watu, kuchoma moto nyumba na maduka, na kusababisha wimbi jipya la wakimbizi wanaokimbia kuokoa maisha yao. Mashirika ya kiraia yameripoti kuwa idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka, kwani wanamgambo hao pia waliwateka nyara baadhi ya wakazi.
Shambulio hili si tukio la pekee, bali ni mwendelezo wa mfululizo wa mauaji ya kikatili ambayo yameitikisa mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi uliopita, Septemba 8, kundi hilohilo lilivamia eneo la Ntoyo, pia katika jimbo la Lubero, na kuua kinyama zaidi ya watu 70 waliokuwa kwenye msiba. Mwezi Agosti, mashambulizi kadhaa katika maeneo ya Beni na Lubero yalisababisha vifo vya raia wasiopungua 52, na mwezi Julai, waumini zaidi ya 40 waliuawa kanisani katika jimbo la Ituri.
Wakati ADF wakiendeleza umwagaji damu, eneo la mashariki mwa Kongo linakabiliwa na janga kubwa zaidi la usalama kutokana na kuwepo kwa zaidi ya makundi 100 ya waasi. Kundi la waasi wa M23, linalodaiwa kusaidiwa na Rwanda, limezidisha hali kuwa mbaya zaidi. Mapema mwaka huu, M23 walitekeleza mashambulizi makubwa na kufanikiwa kuiteka miji muhimu ya Goma (mji mkuu wa Kivu Kaskazini) na Bukavu (mji mkuu wa Kivu Kusini), hatua iliyoleta changamoto kubwa kwa uhuru na mamlaka ya serikali ya Kinshasa.
Jitihada za kidiplomasia za kuleta amani zimeonekana kugonga mwamba. Licha ya serikali ya Kongo kusaini makubaliano ya amani na Rwanda mwezi Juni chini ya upatanishi wa Marekani na Qatar, na kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na M23 mwezi Julai, mapigano bado yanaendelea. Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu aliliambia Baraza la Usalama hivi karibuni kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano hayajakuheshimiwa, na hivyo kuacha mustakabali wa amani katika eneo hilo ukiwa shakani.