Hali ya majonzi na matumaini imetawala katika machimbo ya Nyandolwa, wilayani Shinyanga, ambapo serikali imewahakikishia ndugu wa watu 20 waliofukiwa na kifusi cha mgodi kuwa juhudi za uokoaji bado zinaendelea. Akizungumza na ndugu waliofikwa na maafa, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewasihi kuwa na uvumilivu na matumaini, akisisitiza kuwa serikali inatumia kila mbinu kuwafikia ndugu zao.
Mtatiro ametoa ufafanuzi baada ya baadhi ya ndugu kuomba mgodi huo ubomolewe ili waweze kuchukua miili ya wapendwa wao kwa ajili ya maziko, wakiamini kuwa baada ya siku sita, hakuna uwezekano wa kuwapata wakiwa hai. Hata hivyo, Mtatiro amesema pendekezo hilo haliwezekani kwa kuwa kubomoa mgodi kwa kutumia mitambo mikubwa kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi na kuwaua hata wale ambao pengine bado wapo hai chini ya ardhi.
"Tunaendelea kutumia njia za jadi za uokoaji ambazo ni salama zaidi. Tumeweza kuwapata watu wawili wakiwa hai na mmoja bado anapatiwa matibabu hospitalini," Mtatiro alisema. Aliongeza kuwa, timu ya wataalamu imefanikiwa kubaini walipo watu wengine wawili, na uokoaji wao unatarajiwa kufanyika muda wowote. Watu ambao wameokolewa ni pamoja na Anthony Clement na Mayugula Japhet, huku Flano Peter akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kisurwa, wamefika eneo la tukio kuwafariji ndugu na kusimamia zoezi la uokoaji. Sillo amesisitiza umuhimu wa njia zinazotumika sasa kwani zinatoa fursa ya kuwapata watu wakiwa hai, huku akiahidi kuwa wataendelea kuwa eneo hilo hadi zoezi la uokoaji litakapokamilika.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Kisurwa, ameagiza kuongezwa kwa kasi ya uokoaji, huku akitoa tahadhari na kukataza marekebisho ya migodi kwa njia hatari kama ile iliyosababisha maafa. Ameagiza kwamba matengenezo hayapaswi kufanyika katika sehemu tatu kwa wakati mmoja, kwani huhatarisha maisha ya wachimbaji. Hadi kufikia Agosti 17, 2025, ni siku ya sita tangu watu hao 25 walipofukiwa, ambapo watu watano wametolewa, wawili wakiwa wamefariki, na 20 bado wamekwama.