Hali ya simanzi na taharuki imeendelea kutawala katika eneo la machimbo ya dhahabu ya Nyandolwa, wilayani Shinyanga, ambapo juhudi za uokoaji zinaendelea kwa kasi katika harakati za kuwaokoa wachimbaji 22 ambao bado wamenasa chini ya ardhi. Ajali hiyo ilitokea jana, Agosti 12, 2025, majira ya saa nne asubuhi, baada ya udongo kutitia na kufunika jumla ya watu 25 waliokuwa wakifanya ukarabati wa maduara ya dhahabu.
Hata hivyo, katikati ya majonzi hayo, kumekuwa na chembe ya matumaini baada ya timu za uokoaji kufanikiwa kuwatoa wakiwa hai wachimbaji watatu kati ya sita waliokuwa wamefunikwa katika duara namba 106. Akizungumza leo eneo la tukio, Chifu Inspekta wa mgodi huo, Fikiri Mnwagi, alisema waliweza kufanya mawasiliano ya sauti na watu waliokuwa kwenye duara hilo, jambo lililorahisisha uokoaji wao.
"Juhudi zinaendelea bila kuchoka. Kwa maduara namba 20 lenye watu wanane na namba 103 lenye watu 11, bado hatujafanikiwa kupata mawasiliano nao. Lakini tumechimba duara la ziada ili kurahisisha ufikiaji na tunajaribu kupitisha hewa, maji na chakula," alisema Mnwagi, akionyesha ukubwa wa operesheni inayoendelea.
Viongozi wakuu wa serikali mkoani humo wamefika eneo la tukio kusimamia shughuli za uokoaji. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewasihi wananchi na familia za waathirika kuwa watulivu wakati wataalamu wakiendelea na kazi. Alithibitisha idadi ya watu waliofukiwa na wale walioolewa, akiahidi kuwa serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wote walionasa wanaokolewa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametoa pole kwa familia na kupongeza moyo wa mshikamano ulioonyeshwa na wachimbaji kutoka migodi jirani, ambao wameweka kambi eneo hilo ili kusaidia katika operesheni ya uokoaji. "Nawashukuru sana majirani hawa kwa upendo wao, kwa sababu waokoaji wa kwanza ni wale waliopo karibu na eneo la tukio," alisema Mhita. Juhudi za uokoaji bado zinaendelea huku taifa zima likiwaombea wachimbaji waliosalia.