Wakati taifa la Afghanistan likiwa bado linaomboleza na kujaribu kuwazika wapendwa wao kufuatia matetemeko mawili makubwa yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,200, janga lingine limewakumba. Ripoti kutoka vyanzo vya kimataifa zimethibitisha kutokea kwa tetemeko la tatu lenye nguvu kubwa ndani ya siku tano, likizidisha hofu na sintofahamu nchini humo.
Kituo cha Ujerumani cha Sayansi ya Jiolojia (GFZ) kimeripoti kuwa mtikisiko huo mpya, wenye ukubwa wa 6.2 kwenye kipimo cha Richter, ulipiga eneo la kusini-mashariki mwa nchi usiku wa Alhamisi. Kina cha tetemeko hilo kilikadiriwa kuwa kilomita 10 tu chini ya ardhi, hali inayoongeza ukubwa wa madhara yake. Wakati huo huo, Shirika la Jiolojia la Marekani (USGS) nalo lilirekodi tetemeko hilo katika eneo la mji wa Jalalabad, karibu na mpaka wa Pakistan, likilitaja kuwa na ukubwa wa 5.6.
Tetemeko hili la hivi karibuni linafuatia mitikisiko miwili iliyotangulia, na kufanya hali ya uokoaji kuwa ngumu zaidi. Serikali ya Taliban imetoa takwimu rasmi zinazoonyesha kuwa hadi sasa, takriban watu 2,205 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 3,640 wamejeruhiwa kutokana na matetemeko mawili ya awali. Idadi hii inahofiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwani shughuli za uokoaji zinaendelea na miili mingi bado ipo chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Hasara ya maisha na mali kutokana na tetemeko la tatu bado haijajumuishwa katika takwimu hizi.
Juhudi za uokoaji zinakabiliwa na changamoto kubwa. Ingawa utawala wa Taliban umesema umetuma vikosi maalum vya kijeshi kusaidia, vikosi hivyo vinapata shida kufikia maeneo yaliyoathirika zaidi. Eneo la maafa lina milima mikali na miinuko, na matetemeko yamesababisha maporomoko ya ardhi na mawe, na kufunga barabara nyingi.
Gazeti la The Guardian la Uingereza linaripoti kuwa hali ni mbaya zaidi katika Mkoa wa Kunar, ambapo inakadiriwa kuwa 98% ya majengo yote yameharibiwa au kubomoka kabisa. Takriban watu 84,000 wamepoteza makazi yao na sasa hawana chakula wala mahali pa kujihifadhi, na hivyo kuibua janga kubwa la kibinadamu.