Maafa Ufilipino: Tetemeko la Nguvu 6.9 Lapiga Cebu, Watu 13 Wahofiwa Kufariki

international | Wed Oct 01 2025


Maafa Ufilipino: Tetemeko la Nguvu 6.9 Lapiga Cebu, Watu 13 Wahofiwa Kufariki

Msiba na hofu vimetanda katikati mwa nchi ya Ufilipino baada ya tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 6.9 kwenye vipimo vya Ritcher kupiga eneo hilo usiku, na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Taasisi ya Jiolojia ya Marekani (USGS) ilithibitisha kuwa kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa karibu na jiji la Bogo katika mkoa wa Cebu, kwenye kina kifupi cha kilomita 10 chini ya ardhi, hali iliyoongeza ukubwa wa mtikisiko uliosikika.


Ingawa mamlaka za Ufilipino zilitoa onyo la Tsunami kwa muda mfupi, ilifutwa baadaye baada ya kuthibitishwa kuwa hakuna hatari. Hata hivyo, maafa tayari yalikuwa yametokea nchi kavu, na kuwaacha mamia ya wakazi wakiwa na hofu kubwa. Katika jiji la Bogo, mamia ya wakazi walikesha nje kwenye viwanja vya wazi karibu na kituo cha zima moto, wakihofia kurejea majumbani mwao.


Taarifa kuhusu idadi ya vifo zinatofautiana huku shughuli za uokoaji zikiendelea. Richard Gordon, Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini humo, aliliambia shirika la habari la CNN kuwa takriban watu 13 wanahofiwa kufariki dunia. Wengi wa waliofariki ni pamoja na maafisa watatu wa kikosi cha ulinzi wa pwani na afisa mmoja wa zima moto, waliokandamizwa na jengo la kituo cha michezo katika mji wa San Remigio lililoporomoka walipokuwa wakicheza mpira wa kikapu. Ripoti zingine zinataja vifo vya watu watano, wakiwemo mtoto mmoja.


Picha na video zilizosambaa mitandaoni zimeonyesha ukubwa wa uharibifu. Jengo la maduka lilionekana likiwaka moto, mgahawa wa McDonald's ulitikisika vikali, na kanisa la kihistoria la Katoliki katika mji wa Daanbantayan liliripotiwa kupata uharibifu. Katika tukio jingine la kushangaza, washiriki wa shindano la urembo walionekana wakiruka kutoka jukwaani kwa hofu.


Mamlaka katika mkoa wa Cebu zimetangaza kufunga shule zote na majengo ya serikali leo, Oktoba 1, ili kuruhusu ukaguzi wa usalama. Ufilipino ipo katika eneo la "Pete ya Moto ya Pasifiki," ambalo hukumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.