Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na mataifa ya Magharibi umezidi kuingia doa baada ya Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani kuanzisha rasmi mchakato wa kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa (UN) dhidi ya Iran. Hatua hii kali imechukuliwa kwa madai kuwa Iran imekiuka kwa kiasi kikubwa masharti ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.
Mataifa hayo matatu ya Ulaya yamearifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba yanatumia kipengele maalum kinachojulikana kama 'snapback'. Utaratibu huu ukianzishwa, unatoa siku 30 tu kabla ya vikwazo vyote vya kimataifa dhidi ya Iran, vilivyokuwa vimeondolewa, kurejeshwa kiotomatiki.
Kurejea kwa vikwazo hivyo kutakuwa na athari kubwa kwa Iran. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni pamoja na marufuku ya kununua na kuuza silaha za kawaida, kusitishwa kwa shughuli zote za makombora ya masafa marefu, marufuku ya kurutubisha madini ya urani, na kuzuiliwa kwa mali za watu binafsi na taasisi mbalimbali. Zaidi ya hapo, sekta zake muhimu za kifedha na nishati, hasa mauzo ya mafuta ghafi, zitakabiliwa na ugumu mkubwa.
Uzuri wa utaratibu huu wa 'snapback' kwa mataifa ya Magharibi ni kwamba unazuia matumizi ya kura ya turufu (veto) kutoka kwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kama Urusi na China, ambao ni washirika wa karibu wa Iran. Hii inamaanisha kuwa, ikiwa hakuna azimio jipya litakalopitishwa ndani ya siku 30 kuendeleza msamaha wa vikwazo, vitaanza kutekelezwa moja kwa moja.
Serikali ya Iran imejibu kwa hasira, ikitaja hatua hiyo kuwa "isiyo ya haki na isiyo halali." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameonya kuwa nchi yake itachukua hatua stahiki kujibu. Aidha, wizara hiyo imetishia kusitisha ushirikiano wote na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) iwapo vikwazo vitarejeshwa.
Licha ya kuanzisha mchakato huu, mataifa ya Ulaya yanasisitiza kuwa bado kuna fursa ya diplomasia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, alisema, "Maendeleo ya nyuklia ya Iran hayawezi kuendelea. Hatua hii si mwisho wa diplomasia, tutaendelea na mazungumzo kwa siku 30 zijazo."
Marekani imeipongeza hatua hiyo, huku Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, akisema, "Tunawashukuru washirika wetu Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani kwa uongozi wao. Wameonesha wazi jinsi Iran inavyokiuka makubaliano."
Wakati huohuo, Urusi na China zimepinga vikali hatua hiyo na zimejaribu kuiokoa Iran kwa kuwasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama, zikipendekeza makubaliano ya nyuklia yaongezwe kwa miezi sita ili kutoa nafasi kwa mazungumzo mapya.