Msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza, Mahmoud Bassal, alitangaza kuwa watu wasiopungua 34 waliuawa katika mashambulizi makali ya anga ya Israel yaliyofanyika katika Ukanda wa Gaza kwa siku moja tu, Mei 25.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mwandishi wa habari Hassan Abu Warda, pamoja na watu wengine tisa. Wao waliuawa katika miji ya kaskazini mwa Gaza, Jabalia na Beit Lahia, wakati makazi ya raia na mikusanyiko yaliposhambuliwa kwa mabomu.
Bassel aliliambia shirika la habari la Xinhua kwamba watu wengine 14 waliuawa katika mji wa kusini mwa Gaza, Khan Younis. Wahasiriwa hao walikuwa katika makazi ya raia, mikusanyiko, na wengine walikuwa wapita njia waliokuwa kwenye pikipiki wakati waliposhambuliwa.
Katika eneo la kati la Gaza, kamanda wa ulinzi wa raia wa eneo la Deir al-Balah, Ashraf Abu Nar, na mkewe, waliuawa nyumbani kwao wakati mashambulizi ya mabomu yalipolenga kambi za wakimbizi na makazi ya raia katika mji huo.
Mwanamke mmoja mjamzito aliuawa katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat baada ya hema lake kushambuliwa na jeshi la Israel.
Katika eneo la Al-Karama, kaskazini mwa mji wa Gaza, raia wa Palestina waliokuwa kwenye mkusanyiko walishambuliwa na ndege zisizo na rubani za Israel, na kusababisha vifo. Katika eneo la Tal Al-Hawa, magharibi mwa mji huo, mtu mwingine aliuawa baada ya gari lake kushambuliwa kwa bomu, alisema Bassel.
Siku moja kabla, Mei 24, wafanyakazi wawili wa Palestina wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu waliuawa katika nyumba yao wakati wa mashambulizi ya bomu kwenye Khan Younis.
Kwa upande mwingine, Brigedi ya Al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, lilitangaza Mei 25 kwamba lilifanya operesheni ngumu ya kijeshi dhidi ya wanajeshi wa Israel waliokuwa wamejificha katika nyumba moja katika kijiji cha Al-Qarara, mashariki mwa Khan Younis, kwa lengo la kuwaangamiza.
Kuhusu hilo, jeshi la Israel lilisema kuwa kamanda wa kikosi cha vifaru cha 52 alijeruhiwa vibaya wakati wa mapigano na wapiganaji wa Hamas kaskazini mwa Gaza.
Israel ilizuia kuingia kwa misaada yote, ikiwa ni pamoja na chakula, katika Ukanda wa Gaza mnamo Machi 2, baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya usitishwaji wa mapigano iliyofikiwa mnamo Januari. Kisha, mnamo Machi 18, Israel ilianzisha tena mashambulizi kamili dhidi ya Gaza.
Wizara ya Afya ya Gaza ilitangaza siku hiyo hiyo kwamba watu 3,785 wameuawa na wengine 10,756 wamejeruhiwa katika mapigano hayo hadi kufikia Mei 25.
Serikali inayoongozwa na Hamas huko Gaza ilitangaza Mei 25 kwamba idadi ya waandishi wa habari waliouawa tangu kuanza kwa vita mnamo Oktoba 2023 imefikia 220.