Kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Sala al-Bardawil, ameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti.
Afisa wa Hamas alisema kuwa al-Bardawil na mkewe waliuawa wakati jeshi la Israel lilipofanya mashambulizi ya anga usiku wa kuamkia leo katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel halijatoa maoni yoyote kuhusu taarifa hiyo.
Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo inaendeshwa na Hamas, imesema kuwa watu 32 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza katika masaa 24 yaliyopita. Wizara hiyo pia imesema kuwa angalau wakaazi 700, wakiwemo watoto 200, wameuawa Gaza tangu Israel ilipoanza tena mashambulizi yake.
Israel ilianza tena mashambulizi dhidi ya Gaza mnamo tarehe 18 mwezi huu, ikidai kwamba Hamas ilikuwa imekataa mazungumzo ya kusitisha mapigano. Hamas inakanusha madai hayo na inasema kuwa Israel ilikiuka makubaliano ya awamu ya kwanza ya kusitisha mapigano, ambayo yalikuwa yamepatanishwa na Marekani, Qatar, na Misri.
Israel na Hamas walikubaliana kusitisha mapigano kwa awamu tatu mnamo Januari 15, huku awamu ya kwanza ikiisha tarehe 1 mwezi huu. Israel ilikuwa ikitaka kuongezwa kwa awamu ya kwanza, wakati Hamas ilitaka kuendelea na awamu ya pili, ambayo ingelenga kusitisha mapigano kabisa.
Mvutano katika eneo hilo umeongezeka zaidi kutokana na mapigano makubwa kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon, ambayo ni mapigano makubwa zaidi tangu kusitishwa kwa mapigano mwezi Novemba mwaka jana.