Hali ya sintofahamu na taharuki imetanda katika eneo la mteremko wa mashariki wa Mlima Everest, kufuatia dhoruba kali na isiyo ya kawaida ya theluji kunasa takriban watu 1000, wakiwemo wapanda mlima na watalii. Tukio hili la kutisha limetokea katika kipindi ambacho kwa kawaida huchukuliwa kuwa salama zaidi kwa shughuli za upandaji milima, na kusababisha hofu kubwa ya uwezekano wa maafa ya kibinadamu.
Eneo lililoathirika zaidi ni Bonde la Karma, lililopo upande wa mashariki wa mlima huo kwenye mwinuko wa takriban mita 4,200 kutoka usawa wa bahari. Ripoti kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa mamia ya waokoaji, wakiwemo wananchi wa eneo hilo, wanafanya kazi usiku na mchana katika mazingira magumu ili kuondoa theluji na kufungua njia za kuwafikia watu walionaswa. Hadi kufikia jana, takriban watu 350 walikuwa wamefanikiwa kuokolewa, lakini bado kuna mamia wengine wanasubiri msaada.
Idadi kamili ya watu walioathirika bado haijathibitishwa rasmi, ingawa vyombo vya habari vya ndani vinakadiria kuwa huenda idadi inafikia watu 1000. Haijafahamika wazi iwapo makadirio haya yanajumuisha waongozaji wazawa na wafanyakazi wasaidizi ambao ni muhimu katika safari za upandaji mlima huu mrefu zaidi duniani. Hofu ya kupoteza maisha imeongezeka kutokana na ripoti nyingi za hema kuporomoka chini ya uzito wa theluji na watu wengi kukumbwa na "hypothermia" (hali ya mwili kupoteza joto kupita kiasi). Mamlaka za utalii za eneo hilo zilisitisha uuzaji wa tiketi za kupanda mlima tangu tarehe 4 Oktoba baada ya hali ya hewa kuanza kubadilika.
Ongezeko hili kubwa la wageni katika Mlima Everest lilitokana na sikukuu ndefu ya siku nane nchini China, inayojumuisha Siku Kuu ya Kitaifa na Tamasha la Mwezi, iliyoanza tarehe 1 Oktoba, na kuwavutia watalii wengi kutumia fursa hiyo. Hata hivyo, mnamo tarehe 3 Oktoba, hali ya hewa ilibadilika ghafla na dhoruba ya theluji ilianza katika baadhi ya maeneo. Wakati upande wa mashariki (Tibet) ukikumbwa na theluji kubwa, upande wa kusini mwa mlima huo, nchini Nepal, kulikuwa na mvua kubwa zilizosababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 47 na kubomoa madaraja.
Mlima Everest, unaopatikana kwenye safu za milima ya Himalaya, ndio mlima mrefu zaidi duniani, ukiwa na kimo cha mita 8,848.86 kutoka usawa wa bahari, kulingana na vipimo rasmi vya pamoja vya China na Nepal vya mwaka 2020. Wakati Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania ukiwa ndoto kwa wengi, Everest ndio kilele cha juu kabisa duniani ambacho huwavutia wapandaji wenye uzoefu zaidi.