Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amefyatua maneno makali na kutuma onyo la moja kwa moja kwa Korea Kusini na Marekani, akisema kuwa usalama wa ardhi ya Korea Kusini sasa upo mikononi mwao wenyewe, kauli inayoashiria kuongezeka kwa uhasama katika Rasi ya Korea. Onyo hili kali lilitolewa wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa maonyesho makubwa ya zana za kivita yaliyopewa jina la 'Maendeleo ya Ulinzi-2025' mjini Pyongyang.
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini (KCNA) limeripoti kuwa Kim alitumia jukwaa hilo kulaani vikali kile alichokiita "muungano wa kinyuklia" unaoendelea kati ya Marekani na Korea Kusini. Alidai kuwa nchi hizi mbili zinafanya mazoezi ya kijeshi ya hatari ambayo yanalenga kutekeleza mipango ya mashambulizi ya nyuklia dhidi ya taifa lake. Aliongeza kuwa Marekani inaendelea na mkakati wa kuongeza zana zake za kijeshi nchini Korea Kusini na maeneo jirani, jambo ambalo serikali yake inaliona kama tishio jipya na la moja kwa moja kwa usalama wa taifa.
Katika kuonyesha kwamba Korea Kaskazini haitazami tu, Kim Jong Un alisisitiza kuwa nchi yake imekuwa ikifuatilia kwa umakini mkubwa mienendo yote ya kijeshi ya Marekani, ikiwemo uwekaji wa zana za kimkakati za mashambulizi na upelelezi, na tayari imechukua "hatua zilizo wazi" kujibu vitendo hivyo.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza kwa uwazi kwamba kadri jeshi la Marekani linavyozidi kujiimarisha nchini Korea Kusini, ndivyo na Korea Kaskazini inavyoongeza umuhimu wa kimkakati katika eneo hilo. "Tumezielekeza rasilimali zetu maalum kwenye maeneo muhimu tunayoyalenga kulingana na hali hiyo," alisema Kim, akimaanisha kuwa Korea Kaskazini imeweka silaha zake za kisasa tayari kulenga maeneo maalum ya adui. Alimalizia kwa onyo kali, akisema, "Maadui zetu wanapaswa kutafakari kwa kina kuhusu mwelekeo ambao mazingira yao ya usalama yanaelekea."
Maonyesho ya 'Maendeleo ya Ulinzi' ni jukwaa linalotumiwa na Korea Kaskazini kuonyesha maendeleo yake katika teknolojia ya silaha na zana za kijeshi. Yalianzishwa rasmi mwaka 2023, yakichukua nafasi ya maonyesho ya awali yaliyofanyika mwaka 2021 kwa jina la 'Kujilinda-2021'.