Dunia imepokea habari muhimu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (Korea Kaskazini) ikithibitisha kwa mara ya kwanza rasmi kuwa imetuma vikosi vyake vya jeshi kushiriki katika mapigano ndani ya eneo la Urusi. Tangazo hili la kushangaza limetolewa kupitia gazeti rasmi la chama tawala, Rodong Sinmun, katika fomu ya taarifa ya maandishi kutoka kwa Kamati Kuu ya Kijeshi ya Chama cha Wafanyakazi, iliyochapishwa tarehe 28 Aprili.
Katika taarifa hiyo, Kamati Kuu ya Kijeshi ilisema kuwa "operesheni ya ukombozi wa mkoa wa Kursk" - ikimaanisha eneo la Urusi lililoathiriwa na mapigano - imekamilika kwa "ushindi". Sehemu ya kutia fora katika taarifa hiyo ni kukiri bayana kwamba "vikosi vya jeshi letu," vilivyoagizwa na "Mkuu wa Nchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea," vilishiriki katika operesheni hiyo ya Kursk. Taarifa hiyo iliendelea kusifu askari wake kwa kuonesha "morali ya juu ya mapigano na weledi wa kijeshi." Pyongyang imeyaona matokeo ya operesheni hiyo kama ushindi wa "haki dhidi ya dhuluma" na dhihirisho la "urafiki thabiti wa kivita" pamoja na "uhusiano wa kimkakati wa hali ya juu" uliopo kati ya Korea Kaskazini na Urusi. Pia, walitoa shutuma kali, wakidai kuwa mamlaka ya Ukraine "iliyokuwa mstari wa mbele wa tawala za kibeberu" ilifanya "mauaji ya halaiki ya raia wasio na hatia" katika mkoa wa Kursk.
Aidha, taarifa hiyo imefichua kuwa Mwenyekiti wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alitathmini hali ya mapigano kuwa inakidhi masharti ya kifungu cha 4 cha Mkataba wa Ushirikiano Kamili wa Kimkakati uliotiwa saini kati ya Korea Kaskazini na Urusi mwezi Juni mwaka jana. Kifungu hicho kinasema kuwa iwapo mojawapo ya nchi hizo mbili itajikuta katika hali ya vita, nyingine itatoa msaada wa kijeshi bila kuchelewa. Kulingana na Kamati Kuu ya Kijeshi, Kim Jong Un, akitegemea uchambuzi huu wa kifungu cha 4, alifanya uamuzi wa kutuma vikosi vya jeshi la Korea Kaskazini na kuarifu upande wa Urusi kabla ya kutoa amri ya "ukombozi wa mkoa wa Kursk" kwa Kamati ya Kijeshi.
Kim Jong Un mwenyewe amenukuliwa akielezea ushiriki wa vikosi vyao kama "dhamira takatifu" ya "kuimarisha zaidi urafiki wa jadi" kati ya nchi hizo mbili, "kuhakikisha maendeleo na ustawi wa mataifa yote mawili," na "kulinda heshima ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea." Serikali ya Pyongyang pia imesema inaona ni "heshima" kuwa na uhusiano wa kindugu na "taifa lenye nguvu kama Urusi" na kwamba inajisikia "furaha" kwa kuwa ushiriki wa vikosi vyao umesaidia "kuimarisha zaidi uhusiano wa kivita" na kuchangia katika "utekelezaji wa operesheni maalum ya kijeshi" ya Urusi.
Kukiri huku kwa Korea Kaskazini kunakuja siku chache tu baada ya Urusi mwenyewe kutangaza kuwa vikosi vya Korea Kaskazini vilishiriki katika mapigano. Tarehe 26 Aprili, Urusi ilitangaza kudhibiti kikamilifu jimbo la Kursk, ambalo lilikuwa limetekwa kwa muda na vikosi vya Ukraine. Mkuu wa Majeshi ya Urusi, Jenerali Valery Gerasimov, katika mkutano wa video na Rais Vladimir Putin, alithibitisha kukamilika kwa "operesheni ya ukombozi wa Kursk," akidai kuwa zaidi ya wanajeshi 76,000 wa Ukraine walikufa au kujeruhiwa. Muhimu zaidi, Jenerali Gerasimov alisema, "ningependa kusisitiza jukumu la wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea walioshiriki katika operesheni ya ukombozi wa Kursk." Siku iliyofuata, tarehe 27 Aprili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, pia alizungumzia ushiriki wa vikosi vya Korea Kaskazini, akisema "mshikamano uliooneshwa na marafiki wetu wa Korea Kaskazini unaonesha kiwango cha juu cha muungano kati ya nchi zetu." Maendeleo haya yanaashiria hatua kubwa katika