Hannibal Gaddafi, mtoto wa tano wa aliyekuwa kiongozi wa kimabavu wa Libya, Muammar Gaddafi, hatimaye ameachiwa huru kutoka kizuizini nchini Lebanon. Hii ni baada ya kushikiliwa kwa takriban muongo mmoja katika mazingira tata ya kisheria, akitumikia kifungo bila hata kupandishwa kizimbani na kuhukumiwa.
Shirika la habari la serikali ya Lebanon (NNA) liliripoti Jumanne kuwa Hannibal aliachiwa kwa dhamana. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya wakili wake kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani 893,000, ambacho ni sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 2.3.
Hatua hii ya sasa inakuja baada ya mchakato mrefu wa kisheria na kidiplomasia. Mwezi uliopita, mahakama ya Lebanon ilikuwa imemwamuru Hannibal kulipa dhamana ya mwanzo ya Dola za Kimarekani milioni 11 (kama TZS Bilioni 28.6) na pia ilimwekea marufuku ya kusafiri nje ya nchi. Hata hivyo, hali ilibadilika kufuatia ziara ya ujumbe maalum kutoka Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Libya, ambao walifanya mazungumzo na mamlaka za Lebanon. Matokeo ya mazungumzo hayo yalikuwa ni uamuzi wa mahakama tarehe 6 mwezi huu wa kupunguza kiwango cha dhamana na kumuondolea zuio la kusafiri.
Kesi ya Hannibal Gaddafi imekuwa ikizua utata mkubwa tangu alipokamatwa mwaka 2015. Alikamatwa akituhumiwa kuficha taarifa kuhusu tukio la kihistoria la kupotea kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Kishia nchini humo, Imam Musa al-Sadr, na wenzake wawili. Al-Sadr, ambaye pia alikuwa mwanzilishi wa vuguvugu la kisiasa la 'Amal Movement', alitoweka kimazingara nchini Libya mwaka 1978. Alikuwa amekwenda Libya kwa mwaliko rasmi wa Muammar Gaddafi mwenyewe.
Hoja kuu inayopinga kushikiliwa kwa Hannibal ni ukweli kwamba wakati Imam al-Sadr anapotea mwaka 1978, Hannibal alikuwa mtoto mdogo wa umri wa miaka miwili tu. Hii ilizua hisia kali na madai kwamba amebambikiwa kesi na kutumika kama 'mbuzi wa kafara' au chombo cha kisiasa kutokana na historia ya utawala wa baba yake. Zaidi ya hayo, tofauti na baadhi ya ndugu zake, Hannibal hakuwahi kushika wadhifa wowote wa juu serikalini nchini Libya. Kuonyesha kupinga kwake kushikiliwa bila kesi, mwaka 2023 Hannibal alifanya mgomo wa kususia chakula (hunger strike) uliosababisha afya yake kudhoofika na kulazwa hospitalini kwa matibabu.
Safari ya Hannibal hadi kufika gerezani Lebanon ni ndefu na yenye mikasa. Mwaka 2011, wakati wimbi la "Mvutano wa Kiarabu" (Arab Spring) lilipofika Libya na mji mkuu Tripoli kutekwa na waasi, Hannibal alikimbia na familia yake kwenda nchi jirani ya Algeria. Mwaka 2012 alihamia Oman, na baadaye akapata hifadhi ya kisiasa mjini Damascus, Syria. Ilikuwa ni mwaka 2015, akiwa Syria, ndipo alipotekwa nyara na kundi lenye silaha lisilojulikana na kupelekwa Lebanon, ambako alikamatwa mara moja na mamlaka na kuwekwa kizuizini.
Baba yake, Muammar Gaddafi, alitawala Libya kwa mkono wa chuma kwa miaka 42, baada ya kuingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 1969 akiwa na cheo cha Kapteni jeshini. Alijijengea sifa mbaya kimataifa kwa kufadhili ugaidi, ikiwemo mashambulio ya bomu huko Roma na Vienna mwaka 1985, na shambulio la kutisha la kulipua ndege ya abiria ya Pan Am juu ya Lockerbie, Scotland, mwaka 1988, lililoua watu 270.
Alijulikana pia kwa ufisadi mkubwa, akidaiwa kukusanya utajiri haramu wa takriban Dola za Kimarekani bilioni 200 (zaidi ya TZS Trilioni 520). Alikuwa mpenda anasa na dhahabu; aliripotiwa kumiliki bastola ya dhahabu, taji la dhahabu, na hata sofa za dhahabu ziligunduliwa katika makazi yake. Rais wa zamani wa Marekani, Ronald Reagan, aliwahi kumpachika jina la "Mbwa Mwitu wa Mashariki ya Kati" (Mad Dog of the Middle East).
Mwisho wa utawala wake ulikuja mwaka 2011. Alishindwa kuzuia wimbi la "Mvutano wa Kiarabu". Mwezi Agosti 2011, waasi waliteka Tripoli. Baada ya miezi miwili ya kujificha, mnamo Oktoba 20, alipatikana akiwa amejificha ndani ya bomba la maji taka katika mji aliozaliwa wa Sirte, na kuuawa kikatili kwa kupigwa risasi na wapiganaji waasi.