Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mjadala mkubwa na uvumi uliosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ukiunganisha tukio la nyangumi wanne kukwama ufukweni nchini Japani na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika Rasi ya Kamchatka, Urusi. Wengi wamehoji kama matukio haya yanahusiana, wakiamini kwamba nyangumi hao walionekana kama ishara ya tetemeko lijalo.
Ripoti kutoka gazeti la Asahi Shimbun na vyanzo vingine zimeeleza kuwa, Polisi wa Japani walipokea taarifa mnamo tarehe 29 Julai, majira ya saa kumi na mbili jioni, kuhusu kuonekana kwa nyangumi wanne katika ufukwe wa Tateyama, Mkoani Chiba. Maafisa walithibitisha kuwa nyangumi hao walikuwa hai na kila mmoja alikuwa na urefu wa takriban mita 7 hadi 8.
Hali ilibadilika na uvumi kuongezeka punde baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 8.8 kutokea katika Rasi ya Kamchatka asubuhi ya siku iliyofuata, yaani tarehe 30 Julai, saa mbili na dakika ishirini na tano asubuhi. Watumiaji wa mitandao ya kijamii walihusisha moja kwa moja kuonekana kwa nyangumi hao na tetemeko hilo, wakidai kuwa ni ishara ya mapema ya tukio la kijiolojia.
Mtaalamu mmoja kutoka Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Sayansi nchini Japani alieleza kuwa nyangumi hao wanaonekana kuwa wa jamii ya nyangumi wenye mafuta (sperm whales), ambao huonekana mara kwa mara katika eneo la Tateyama. Hata hivyo, alibainisha kuwa kuonekana kwa nyangumi wanne kwa pamoja ni jambo lisilo la kawaida na la kwanza kushuhudiwa. Aliongeza kuwa hakuna uhakika wa moja kwa moja iwapo sauti zisizo za kawaida chini ya bahari kabla ya tetemeko zinaweza kuwa ziliwaathiri nyangumi hao, jambo ambalo linaibua maswali mengi.
Hata hivyo, gazeti la Asahi Shimbun lilisisitiza kuwa "ni vigumu kuthibitisha matukio kama hayo na uchunguzi wa kina wa eneo unahitajika ili kubaini chanzo." Gazeti hilo pia lilikumbusha tukio kama hilo la mwaka 2011, ambapo wiki moja kabla ya tetemeko kubwa la ardhi la Mashariki mwa Japani, zaidi ya pomboo 50 wa jamii ya 'melon-headed whales' walikwama ufukweni mkoani Ibaraki, kusini mwa Fukushima. Utafiti uliofanywa na timu ya watafiti wa chuo kikuu ulihitimisha kuwa hakukuwa na uhusiano wowote kati ya tukio la pomboo na tetemeko la ardhi.
Mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali linalochunguza nyangumi wanaokwama ufukweni alifafanua kuwa ni kawaida kwa nyangumi mmoja au zaidi kuonekana ufukweni kila siku. Kwa hiyo, alisisitiza kuwa "hakuna ushahidi wa kutosha kuamini kwamba haya ni ishara za tetemeko la ardhi." Kauli hii inatoa mwangaza na kupunguza hofu na uvumi usiokuwa na msingi, ikikumbusha umuhimu wa kuzingatia ukweli wa kisayansi badala ya kuamini hisia au hadithi zisizothibitishwa. Ni muhimu kwa wananchi wa Tanzania na kwingineko kuelewa kuwa matukio haya ya kiasili mara nyingi huendana na sababu za kibiolojia au mazingira, badala ya kuwa viashiria vya majanga.