Kuna mzozo mkubwa wa kisiasa na kijeshi unaondelea Mashariki ya Kati, huku kiongozi wa wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon, Na’im Qassem, akitoa msimamo mkali, akisema kikundi chake hakitaweka silaha chini maadamu Israel inaendelea na mashambulizi yake. Qassem ametoa onyo kali, akisema, "Kama Israel itazindua mashambulizi makubwa dhidi ya Lebanon, basi kutakuwa na vita vipya." Msimamo huu unaweza kuongeza sintofahamu na kuleta vita vikali zaidi katika eneo hilo.
Katika hotuba yake iliyotangazwa kwenye televisheni, Katibu Mkuu wa Hezbollah, Qassem, alisisitiza kuwa kikundi chake hakitaacha silaha wakati "silaha zote za nguvu ziko mikononi mwa adui, Israel." Maneno haya yanakuja wakati ambapo Serikali ya Lebanon inashinikizwa na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Marekani, kuishinikiza Hezbollah iweke silaha chini. Kauli yake inaonyesha wazi kwamba Hezbollah inaona kuwa silaha zao ni ulinzi pekee dhidi ya vitisho vya Israel.
Mgogoro huu umejengeka baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mapigano kati ya Hezbollah na Israel, kufuatia mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 8, 2023. Ingawa Hamas ilikumbana na pigo kubwa, ikiwemo kupoteza viongozi wake wakuu na kuharibiwa kwa silaha zake, Hezbollah ilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel mwezi Novemba 2024. Hata hivyo, mivutano bado inaendelea, na hatima ya Lebanon inabaki mashakani.
Baada ya Hamas kupungua nguvu, pia imeonekana kuwa ushawishi wa Hezbollah ndani ya Lebanon umepungua. Marekani na Lebanon wamekuwa katika mazungumzo tangu Juni mwaka huu kuhusu uwezekano wa Hezbollah kuweka silaha chini, ili Israel isitishe mashambulizi yake ya angani, lakini hakuna maendeleo makubwa yaliyofanyika.
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ameongeza sauti yake akitaka Hezbollah iweke silaha chini. Katika hotuba yake ya Siku ya Jeshi la Lebanon, Aoun alisema kuwa "Lebanon iko katika hatua muhimu," na inapaswa kuchagua kati ya "kuanguka au utulivu." Aoun anaunganisha msaada wa kimataifa kwa Lebanon na uwezekano wa Hezbollah kuweka silaha zake chini, ishara kwamba serikali inaona silaha za Hezbollah kama chanzo cha matatizo na sio utulivu.