Mfululizo wa vitendo vya chuki na dharau za kidini umeikumba Ufaransa baada ya vichwa vya nguruwe kuachwa kimakusudi mbele ya misikiti kadhaa katika jiji la Paris na maeneo ya jirani. Kitendo hicho, ambacho ni dharau kubwa kwa Waislamu kwani nguruwe anachukuliwa kuwa mnyama najisi, kimetajwa na mamlaka kama uhalifu wa chuki, huku uchunguzi ukionesha kuwa ni njama iliyopangwa na watu kutoka nje ya nchi.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Paris imetangaza kuwa wahusika wa vitendo hivyo ni raia wa kigeni ambao walitoroka Ufaransa mara tu baada ya kutekeleza uhalifu wao kati ya usiku wa Septemba 8 na alfajiri ya Septemba 9. Katika baadhi ya maeneo, vichwa hivyo viliwekwa ndani ya mabegi ya safari, na kichwa kimoja kilikutwa kimeandikwa jina la Rais wa Ufaransa, "Macron," kwa wino wa bluu.
Uchunguzi ulipata nguvu baada ya mkulima mmoja kutoka eneo la Normandy kuripoti kuwa watu wawili walinunua takriban vichwa kumi vya nguruwe kutoka kwake, na alishuku kuwa namba za usajili za gari lao zilikuwa za Serbia. Kwa kutumia video za CCTV, polisi walithibitisha kuwa washukiwa walitumia gari hilo kuingia Paris na walinaswa wakiweka vichwa hivyo mbele ya misikiti. Ufuatiliaji wa laini ya simu ya Kikroeshia waliyokuwa wakitumia ulionesha walivuka mpaka na kuingia Ubelgiji mara baada ya tukio.
Hata hivyo, mamlaka za Ufaransa zinaamini kuwa tukio hili si la chuki la kawaida, bali ni njama ya kigeni yenye "nia ya wazi ya kuzua migawanyiko na machafuko ya ndani," kama alivyosema mwendesha mashtaka. Mkuu wa Polisi wa Paris, Laurent Nuñez, naye alidokeza juu ya "uwezekano wa kuingiliwa na nchi za kigeni."
Ingawa hawajataja nchi yoyote rasmi, lawama nyingi zinaelekezwa kwa Urusi. Mashaka haya yanatokana na tukio la awali la Oktoba 2023, baada ya kuanza kwa vita kati ya Israeli na Hamas, ambapo alama za "Nyota ya Daudi" za Wayahudi zilichorwa kwenye majengo mbalimbali jijini Paris. Idara ya Usalama wa Ndani ya Ufaransa (DGSI) ilihitimisha kuwa operesheni hiyo iliendeshwa na idara ya ujasusi ya nje ya Urusi (FSB).
Wakati huo, wachambuzi walisema lengo la Urusi lilikuwa ni kuchochea chuki kati ya jamii za Wayahudi na Waislamu nchini Ufaransa, ambao wana idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya, na hivyo kuivuruga nchi kijamii. Inaonekana mbinu hiyo imetumika tena, safari hii ikiwalenga Waislamu moja kwa moja ili kuzua ghadhabu na machafuko.