Gari linalodhaniwa kuwa sehemu ya msafara wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, aina ya 'Aurus Senat', lililipuka na kushika moto mkubwa katika mji wa Moscow mnamo Machi 29.
Tukio hilo lilitokea katika mtaa wa kaskazini wa Lubyanka, karibu na makao makuu ya Shirika la Usalama la Shirikisho la Urusi (FSB). Gari hilo lililolipuka, 'Aurus Senat', ni sedan ya Kirusi isiyopenywa na risasi, na inakadiriwa kuwa na thamani ya takriban Shilingi za Kitanzania bilioni 1.17 (takriban Dola za Kimarekani 400,000). Moto huo ulizimwa haraka, na hakuna majeruhi au vifo vilivyoripotiwa kutokana na mlipuko huo. Hata hivyo, chanzo cha mlipuko bado hakijajulikana.
Hivi karibuni, Rais Putin ameonekana akiongeza hatua za kiusalama. Wakati wa ziara yake huko Murmansk, ilishuhudiwa wanajeshi wa heshima wakikaguliwa kwa kina na maafisa wa Huduma ya Ulinzi ya Shirikisho (FSO). Pia, inaripotiwa kuwa amekuwa akionekana katika maeneo ya umma akiwa amevaa vesti isiyopenywa na risasi, kama hatua ya kujikinga dhidi ya tishio lolote la mauaji.
Mlipuko huu umetokea muda mfupi baada ya Ukraine kutoa kauli isiyothibitishwa ikisema "Putin atakufa hivi karibuni," jambo ambalo limezua uvumi miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda Ukraine inahusika na tukio hilo. Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha madai haya.
Serikali ya Urusi bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hili, na uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mlipuko huo na kama ulikuwa ni jaribio la kumdhuru Rais Putin au ajali tu. Tukio hili linaongeza hali ya wasiwasi katika anga za kisiasa, hasa kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.