EU Yaadhimisha Miaka 50 ya Ushirikiano na Tanzania kwa Kutilia Mkazo Nishati Mbadala

international | Fri May 23 2025


EU Yaadhimisha Miaka 50 ya Ushirikiano na Tanzania kwa Kutilia Mkazo Nishati Mbadala

Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, kwa kushirikiana na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa EU, leo wamefanya maadhimisho ya Siku ya Ulaya kwa mwaka 2025. Katika sherehe hizo, wamekumbuka miaka hamsini ya ushirikiano uliopo kati ya EU na Tanzania, pamoja na miaka ishirini na mitano ya uhusiano mzuri kati ya EU na Umoja wa Afrika. Tukio hili limeangazia ushirikiano wa kimkakati unaozidi kuimarika baina ya EU na Tanzania.


Maadhimisho ya mwaka huu yamejikita hasa katika eneo la Nishati Mbadala na msaada ambao EU inatoa katika sekta hii muhimu. Upataikanaji wa nishati safi ni jambo la msingi kwa maendeleo endelevu ya Tanzania, ukuaji wa uchumi wake, na uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hafla hiyo imewakutanisha Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, mabalozi wa EU, maafisa mbalimbali wa serikali ya Tanzania, vijana, wanahabari, na wanadiplomasia wengine.


Katika hotuba yake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Bi. Christine Grau, alielezea kwa kina kuhusu ushirikiano uliopo kati ya EU na Tanzania. Alisema: “Ushirikiano wetu unaendelea kukua na kuwa wa kimkakati zaidi, ukijengwa juu ya maslahi yetu ya pamoja na ustawi wa pande zote mbili. Sisi si wafadhili tu, bali ni washirika wa kweli. Kupitia mkakati wa Global Gateway, tunaunga mkono juhudi za Tanzania katika nishati mbadala, masuala ya kidigitali, uongezaji thamani wa bidhaa, na miundombinu endelevu.”


Mheshimiwa Kombo alishukuru kwa msaada endelevu unaotolewa na Umoja wa Ulaya, hasa katika sekta ya nishati. Alipongeza EU kwa kuoanisha ushirikiano wake na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050.


Kupitia mpango wa Global Gateway, Timu ya Ulaya imeahidi kutoa kiasi cha Euro milioni 990 (ambayo ni zaidi ya Shilingi trilioni 3 za Kitanzania) kwa ajili ya kusaidia sekta ya nishati nchini Tanzania. Msaada huu unajumuisha mchango wa moja kwa moja wa Euro milioni 191.9 (sawa na takribani Shilingi bilioni 565 za Kitanzania) kutoka EU kwa ajili ya nishati safi na kuunganisha mifumo ya nishati ya mipakani. Baadhi ya miradi mikubwa inayofadhiliwa ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono (wenye thamani ya Euro milioni 299, takribani Shilingi bilioni 880 za Kitanzania), ambapo EU inachangia Euro milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 106 za Kitanzania). Pia, EU inashiriki katika miradi ya kuunganisha mifumo ya nishati na nchi za Zambia na Uganda, yenye thamani ya Euro milioni 604.4 (takribani Shilingi trilioni 1.8 za Kitanzania).


EU pia inaunga mkono matumizi ya majiko safi kwa kuwekeza kiasi cha Euro milioni 30 (takribani Shilingi bilioni 88 za Kitanzania) na ina mpango mpya wa kikanda wa Euro milioni 20 (takribani Shilingi bilioni 59 za Kitanzania) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa suluhisho za nishati safi. Uwekezaji zaidi katika miundombinu ya nishati kwa ajili ya sekta za kilimo na madini unaendelea.


Ushirikiano huu hauhusu tu miundombinu. Wageni waliohudhuria Siku ya Ulaya walikutana na wanawake vijana wa Kitanzania wanaosoma masomo yanayohusiana na nishati – ambao wamenufaika na ufadhili wa masomo kutoka EU, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na Ubalozi wa Ireland. Mnamo Novemba mwaka 2024, ufadhili wa masomo 25 ulitolewa katika fani ya uhandisi wa nishati endelevu, na kufanya idadi ya wanafunzi wanaofadhiliwa kufikia 35. Mpango huu, ambao ni sehemu ya Mpango wa Kwanza wa Tanzania wa Ufanisi wa Nishati, unalenga usawa wa kijinsia katika sayansi na teknolojia na kusaidia mabadiliko jumuishi kuelekea uchumi wa kijani.


Balozi Grau aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita, msaada wa EU wa Euro milioni 65 (takribani Shilingi bilioni 192 za Kitanzania) umewezesha zaidi ya theluthi moja ya vijiji nchini Tanzania kuunganishwa na umeme, na hivyo kuboresha upatikanaji wa nishati kwa zaidi ya watu milioni moja wanaoishi vijijini. EU inatarajia kuanza awamu mpya ya ushirikiano mwaka 2026, ambao utaendana na Dira ya Maendeleo ya 2050, na utazingatia zaidi ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ukuaji endelevu, ajira kwa vijana, na utawala bora wa kidemokrasia. EU itaendelea kuwa mshirika mkuu wa Tanzania katika biashara, uwekezaji, na maendeleo, ikizingatia amani, ustawi, na maendeleo jumuishi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.