Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameeleza wasiwasi wake kuhusu kizazi cha sasa cha wanafunzi, akisema wengi wanaomaliza masomo yao, kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu, wanashindwa kujitegemea hata kwa mambo madogo kama kufua nguo zao wenyewe.
Dk. Biteko amesema hali hii ni hatari kwa taifa, kwani miongoni mwa wahitimu hao, kuna watu ambao wanatarajiwa kuwa viongozi na watumishi wa umma. Lakini, kutokana na kushindwa kujitegemea, wanaweza kuwa mzigo kwa jamii badala ya kuihudumia.
Akizungumzia suala la wanafunzi wa vyuo vikuu kwenda kusoma katika vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), Dk. Biteko alisema kuwa nchi isipowekeza katika elimu ya ufundi stadi, italazimika kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa. Hali hii itasababisha nchi kuwa tegemezi katika kila sekta ya uzalishaji.
Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini.
“Ni jambo la kawaida kuona kijana anamaliza kidato cha sita au hata ana shahada, lakini hawezi kufua nguo zake mwenyewe. Anahitaji kufanyiwa kila kitu,” alisema Dk. Biteko.
“Siku moja, nilipewa mwaliko na Waziri wa Elimu kwenye mkutano wa wamiliki wa shule binafsi. Niliwapa changamoto kwamba wanazalisha maofisa wa kuhudumiwa badala ya watu ambao wataenda kuhudumia jamii. Hili ni jambo hatari kwa taifa na linahitaji kuangaliwa kwa umakini. VETA mna nafasi kubwa ya kusaidia kuhakikisha watoto tunaowafundisha leo, wanapomaliza kidato cha nne au cha sita, wanakuwa na ujuzi ambao utawasaidia kujitegemea na kukabiliana na mazingira yao,” aliongeza.
Dk. Biteko alisisitiza kuwa elimu ya ufundi stadi ni eneo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele ili kuwawezesha watoto kujitegemea baadaye. Aliitaka VETA kuanza kutumia teknolojia mpya zinazoibuka katika mifumo ya ufundishaji ili kuwasaidia vijana kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Alisema serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya na mkoa nchini ili kupunguza tatizo la ajira, kuongeza kipato cha watu, na kuzalisha watumishi ambao wataisaidia jamii badala ya kuwa tegemezi.
“Katika dunia ya sasa, uwekezaji katika ufundi stadi ni muhimu sana. Unatoa uhakika wa kupata faida kubwa kutokana na uwepo wa vijana wengi wanaojishughulisha na uzalishaji,” alisema Dk. Biteko.
Akizungumzia kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu kwenda kusoma VETA, Dk. Biteko alisema, “Nataka niwaambie, hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na watu wenye ujuzi wa kutatua matatizo yao. Tukishindwa kuwekeza katika kuwafundisha watoto wetu ujuzi huu, tutalazimika kuutafuta nje ya nchi kwa gharama kubwa. Matokeo yake, kazi zote, iwe ni kujenga barabara au nyumba, zitakuwa na gharama kubwa kwa sababu ujuzi huo hautapatikana ndani ya nchi, na hii itatuingizia hasara kubwa.”
Dk. Biteko aliongeza kuwa sekta binafsi inapaswa kushirikiana na serikali katika kuzalisha watumishi ambao watajenga taifa, badala ya kutoa watu ambao wanaendelea kuwa tegemezi baada ya kuhitimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema maadhimisho hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vya VETA na wazalishaji katika maeneo ya kazi.
“Tumeanza kuhakikisha kwamba tunachofundisha kwenye vyuo vyetu kinaendana na mahitaji ya wazalishaji,” alisema Profesa Mkenda.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Antony Kasore, alisema maadhimisho hayo yalifanyika kwa siku nne kuanzia Machi 18, mwaka huu, na yalijumuisha maonesho ya bidhaa za ubunifu, mashindano ya ujuzi yaliyoshirikisha wanafunzi 16 kutoka nchi nzima, na makongamano kuhusu ufundi stadi na ubunifu.