Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, ametangaza kuwa serikali yake inapanga kujaribu kuinunua tena Bandari ya Darwin, bandari muhimu iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo ambayo kwa sasa imekodishwa kwa muda mrefu kwa kampuni moja ya China. Hatua hii inakuja kutokana na wasiwasi unaoongezeka nchini Australia kuhusu usalama wa taifa na udhibiti wa mali muhimu na kampuni za kigeni, hasa zile zinazohusishwa na serikali ya China.
Akizungumza katika mahojiano ya redio, Bwana Albanese alisema kuwa Bandari ya Darwin ni "rasilimali ya kimkakati" na ni matakwa ya serikali yake kuona inarudi mikononi mwa Waustralia. Aliongeza kuwa serikali yake itaanzisha mazungumzo yanayolenga kufanikisha hilo.
"Tunaishi katika ulimwengu usio na uhakika kwa sasa," alisema Waziri Mkuu Albanese, akisisitiza kuwa "wazo la bandari kuu katika eneo la kaskazini mwa Australia kumilikiwa na kampuni ya kigeni halifai maslahi ya kitaifa ya Australia."
Alifichua kuwa serikali imekuwa ikiandaa mipango ya kuhakikisha kuwa bandari hiyo inarudi kwa Waustralia, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na wanunuzi wanaoweza kujitokeza. Aliongeza kuwa "wakati utakapofika ambapo serikali ya shirikisho ya Australia inahitajika kuingilia kati moja kwa moja, tutakuwa tayari kufanya hivyo."
Bwana Albanese pia alizungumzia uwezekano wa kushirikisha mifuko ya pensheni ya kibinafsi katika ununuzi huo ili kupunguza mzigo kwa walipa kodi. Hata hivyo, aliongeza kuwa serikali iko tayari kutumia fedha za umma ikiwa ni lazima ili kuhakikisha kuwa Bandari ya Darwin inakuwa mali ya taifa.
Mnamo mwaka 2015, serikali ya Jimbo la Northern Territory iliikodisha Bandari ya Darwin kwa kampuni ya Kichina iitwayo Landbridge kwa muda wa miaka 99 kwa takriban dola za Australia milioni 500 (takriban TZS 1.25 trilioni kwa viwango vya sasa vya ubadilishaji).
Tangu wakati huo, uhusiano kati ya Australia na China umeharibika kwa kasi. Pia, kuibuka kwa taarifa zinazohusisha Landbridge na Chama cha Kikomunisti cha China kumezua hofu kubwa nchini Australia kuhusu masuala ya usalama. Wito umetolewa mara kwa mara wa kutaka mkataba huo ubatilishwe.
Wakati mkataba huo uliposainiwa, Rais wa wakati huo wa Marekani, Barack Obama, alikosoa serikali ya Australia kwa kutowajulisha Marekani mapema kuhusu mpango huo, hasa ikizingatiwa kuwa kuna kambi ya wanajeshi wa Marekani (US Marines) iliyoko Darwin.
Shirika la habari la Bloomberg liliripoti mnamo Novemba mwaka jana kuwa Landbridge ilikuwa inakabiliwa na matatizo ya kifedha. Baada ya hapo, serikali ya Australia na serikali ya Northern Territory zimekuwa zikijadili mbinu za kukabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika inayozunguka bandari hiyo.
Baada ya ripoti kuibuka mwezi uliopita kuhusu uwezekano wa Australia kuinunua bandari hiyo, Landbridge ilitoa taarifa ikisema kuwa haki ya kukodisha Bandari ya Darwin haikuuzwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Albanese alizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa Australia unaotarajiwa kufanyika Mei 3. Alisema kuwa iwapo chama chake cha Labour kitashinda, atafanya kila awezalo kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, "haraka iwezekanavyo." Aliongeza kuwa "tutazungumza kwa uangalifu na kidiplomasia."
Alieleza kuwa maafisa wa Australia tayari wamekuwa wakiwasiliana na upande wa Marekani na kufanya mazungumzo kuhusiana na hatua ya Rais Trump kutangaza ushuru wa pande zote. Hata hivyo, hakufafanua zaidi kuhusu yaliyojadiliwa.
Serikali ya Marekani ilikubali kuiwekea Australia ushuru wa "msingi" wa asilimia 10 pekee, ambao unatumika kwa nchi nyingine duniani. Hata hivyo, Australia inaona kuwa si sahihi kwa Marekani kuiwekea ushuru wakati Australia ina nakisi ya biashara na Marekani.