Takribani watu 16 wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya katika ajali mbaya iliyotokea nchini China, ambapo sehemu ya daraja la reli lililokuwa linajengwa liliporomoka ghafla. Tukio hilo la kusikitisha limeweka wazi hatari za kazi za ujenzi na kuibua maswali mengi kuhusu viwango vya usalama katika miradi mikubwa nchini humo.
Kulingana na ripoti kutoka tovuti ya habari ya China, Zhonghua.net, ajali hiyo ilitokea alfajiri ya Agosti 22, 2025, katika mkoa wa Qinghai, wilaya ya Jianzha. Sehemu ya daraja hilo la reli ilianguka ghafla, na kusababisha vifo vya wafanyakazi 12 waliokuwa wakifanya kazi usiku. Hadi sasa, wafanyakazi wengine wanne bado hawajulikani waliko na wanaaminika kuwa waliangukia mto mkuu wa njano, unaojulikana kama Mto Huang He. Vifaa vya ulinzi kama vile mikanda ya usalama na nyavu za ulinzi vilivyotumiwa na wafanyakazi viliporomoka pamoja na daraja, na kufanya juhudi za uokoaji kuwa ngumu zaidi.
Rekodi za kamera za CCTV zilionyesha wazi jinsi miundo ya chuma ilivyoporomoka ghafla, huku ikitokea cheche nyingi. Watu waliokuwa wakiishi karibu na eneo la tukio walisema walihisi mitikisiko mikubwa kiasi kwamba walidhani kumetokea tetemeko la ardhi. Kelele kubwa ya kuporomoka ilisikika kwa takribani sekunde 10, na kuwalazimu baadhi ya wakazi kukimbia nje kwa hofu.
Kufuatia tukio hilo, Serikali ya Mkoa wa Qinghai iliunda mara moja kituo cha dharura ili kuratibu shughuli za uokoaji na uchunguzi. Mamlaka imetuma vikosi vikubwa vya uokoaji, ikiwemo magari 91 ya uokozi, boti 27, helikopta moja, roboti tano, na jumla ya wafanyakazi 806 ili kutafuta waathirika. Urefu wa daraja lililoporomoka ni kati ya mita 80 hadi 100.
Daraja hilo la reli, ambalo linapita juu ya Mto Huang He, ndilo daraja la kwanza la aina yake kujengwa. Lilikuwa na urefu wa jumla ya mita 1,596 na urefu kutoka usawa wa maji hadi juu kabisa ulikuwa mita 130. Imedokezwa kuwa huenda ajali hiyo ilisababishwa na juhudi za kukamilisha ujenzi kabla ya tarehe iliyopangwa ya kumalizika kwake, ambayo ilikuwa mwezi huu. Baadhi ya wachambuzi wanasema shinikizo la kukamilisha mradi kwa haraka huenda lilisababisha hatua za usalama kusahaulika au kutotekelezwa kwa ukamilifu.