Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) umetoa wito kwa walimu wote wanaojitolea katika shule za serikali nchini kusitisha mara moja utendaji wao. Hatua hii inalenga kuonyesha uhaba mkubwa wa ajira katika sekta ya elimu na kuisukuma serikali kuchukua hatua za haraka za kuajiri walimu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Katibu wa NETO, Daniel Edgar, alieleza kuwa walimu wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea kwa muda mrefu, huku wengine wakilipwa mishahara midogo isiyotosha au kutolipwa kabisa. Alisema hali hii inatoa picha isiyo sahihi kwa serikali, ikionyesha kana kwamba kuna idadi ya kutosha ya walimu, hivyo kupunguza uharaka wa kuchukua hatua za ajira.
"Tunatoa wito kwa wanachama wetu na walimu wote wasio na ajira nchini kuacha mara moja kujitolea katika shule za umma. Hii ndio njia pekee ya kuonyesha uhitaji halisi uliopo," alisisitiza Edgar.
Alifafanua kuwa baadhi ya walimu wanaojitolea wamekuwa wakipokea posho ndogo kiasi cha Shilingi 70,000 za Kitanzania kwa mwezi, wakati wengine wakifanya kazi bila malipo yoyote. Hali hii inawakatisha tamaa walimu wanaotafuta ajira za kudumu na inazidisha tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa wahitimu wa ualimu.
NETO pia imeiomba serikali kuhakikisha kuwa wahitimu wote wa ualimu waliohitimu kati ya mwaka 2015 na 2024 wanapewa ajira rasmi bila kuwekewa masharti yoyote magumu. Edgar alikosoa utaratibu wa sasa wa serikali wa kuwafanyia usaili walimu ambao wamekaa muda mrefu bila ajira, akisema kuwa wanapaswa kuajiriwa moja kwa moja ili kukabiliana na uhaba wa walimu unaoikumba nchi.
"Kundi hili la walimu limekuwa likisubiri ajira kwa miaka mingi. Tunapinga vikali kufanywa kwa usaili kwao, kwani tayari wameshakidhi vigezo vya kitaaluma na wana haki ya kuajiriwa mara moja," alieleza Edgar.
Aidha, NETO imetoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya kusimamia masuala ya mishahara katika shule binafsi. Edgar alibainisha kuwa kuna tofauti kubwa sana ya mishahara inayolipwa walimu wenye taaluma sawa kulingana na ngazi tofauti za elimu wanazofundisha. Alisema usimamizi wa serikali unahitajika ili kuhakikisha kuwa mishahara inalingana na elimu na uzoefu wa mwalimu, hatua ambayo itasaidia kuongeza motisha na ufanisi katika kazi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NETO, Agnes Japhet Mpundi, alionya kuhusu athari za ukosefu wa ajira kwa walimu akisema kuwa inaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine ya kijamii. Alieleza kuwa vijana waliohitimu masomo ya ualimu lakini hawapati ajira hukumbana na changamoto nyingi za kimaisha, ambazo zinaweza kuwashawishi kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.
"Serikali isipochukua hatua za haraka, tunaweza kujikuta tunazalisha wahitimu wengi ambao wanageuka kuwa tatizo kwa jamii. Ni muhimu kuwapa ajira ili waweze kuchangia katika maendeleo ya taifa," alionya Mpundi.
Mpundi pia alihoji ni kwa nini serikali imekuwa na ugumu wa kuajiri walimu licha ya kuwepo kwa ongezeko la mapato katika awamu ya sita. Alilinganisha hali hiyo na utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo alisema walimu wengi waliweza kuajiriwa kwa wakati mmoja hata wakati mapato ya taifa yalipokuwa machache.
NETO imesisitiza kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua za dharura ili kuhakikisha kuwa walimu wote waliohitimu wanapata ajira rasmi, hatua ambayo itaongeza ubora wa elimu nchini na kuepusha athari hasi zinazoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa ajira kwa walimu.