Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imetumia Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) kama jukwaa la kuwasogezea wafugaji teknolojia za kisasa na za gharama nafuu, zinazolenga kuongeza tija na kukabiliana na changamoto sugu katika sekta ya mifugo, hasa uhaba wa malisho wakati wa kiangazi.
Akizungumza katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Profesa Erick Komba, amesema taasisi yake imejipanga kikamilifu kushirikiana na wafugaji wote nchini ili kuhakikisha wananufaika na tafiti na teknolojia zinazobuniwa na wataalamu wa ndani. "Milango yetu ipo wazi. Tupo hapa Sabasaba kutoa elimu na kusambaza teknolojia zetu, ikiwemo mbegu bora za malisho na mbinu za kisasa za ufugaji, ili kuinua mchango wa sekta hii kwenye pato la Taifa," alisema Prof. Komba.
Kivutio kikubwa katika banda la TALIRI ni teknolojia rahisi ya "boksi la kufungia majani," ambayo ni suluhisho la moja kwa moja kwa tatizo la ukosefu wa malisho wakati wa kiangazi. Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki, Dkt. Zabron Nziku, alifafanua kuwa kifaa hiki kinamwezesha mfugaji wa aina yoyote kutengeneza marobota ya majani makavu ('hay') kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
"Hii ni teknolojia rafiki kwa mfugaji. Watu wawili tu wanaweza kutengeneza marobota 350 kwa mwezi, na robota moja linaweza kulisha ng'ombe wawili kwa siku. Hii inamaanisha mfugaji anaweza kuvuna na kuhifadhi chakula cha mifugo kitakachomsaidia sana wakati wa uhaba," alieleza Dk. Nziku.
Mbali na boksi hilo, TALIRI pia inatoa elimu na kuuza mbegu bora za malisho zinazokomaa haraka na kustahimili ukame, pamoja na kutoa ushauri kuhusu mbari bora za mifugo zinazoweza kuleta faida zaidi kwa mfugaji.
Meneja wa Uhaulishaji wa Teknolojia wa taasisi hiyo, Gilbert Msuta, amewakaribisha wafugaji wote na wadau wa mifugo wanaotembelea maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la TALIRI ili kujifunza kwa vitendo na kujipatia teknolojia hizi zitakazowasaidia "kuzalisha kwa tija."