Licha ya jitihada za serikali, changamoto ya nishati bado ni mzigo mkubwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo zaidi ya milioni 940 hawana uhakika wa umeme. Nchini Tanzania pekee, zaidi ya watu milioni 36 (zaidi ya nusu ya wananchi) bado wanakosa umeme na wengi wao hulazimika kutumia nishati hatarishi kama kuni, mkaa na mafuta ya taa kwa ajili ya kupikia na mwanga.
Athari za kukosa nishati safi huangukia zaidi kwa wanawake, ambao hutumia muda mwingi kukusanya kuni na kuvuta moshi wenye sumu wakati wa kupika, jambo linaloathiri afya zao na kuwanyima fursa za kujitafutia kipato.
Suluhisho Kupitia Uwezeshaji wa Wanawake
Katika kukabiliana na changamoto hii ya kitaifa, Puma Energy Foundation imeunganisha nguvu na shirika la Solar Sister, ambalo lina utaalamu katika kuwawezesha wanawake kuanzisha biashara za kuuza bidhaa za nishati safi kama vile taa za sola na majiko safi.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, Solar Sister imeunda mtandao wa wajasiriamali wanawake zaidi ya 12,000 katika ukanda huo, wakiwafikia watu zaidi ya milioni 5.5. Nchini Tanzania, mpango huu umefikia zaidi ya watu milioni 2.3 tangu ulipoanzishwa mwaka 2013, ukibadilisha maisha ya maelfu ya wanawake vijijini. Wajasiriamali hawa hupewa mafunzo ya masoko, uhasibu, mipango ya biashara, na upatikanaji wa mikopo midogo.
Awamu ya Pili Kutanua Wigo: Mafunzo na TEHAMA
Ushirikiano huu umepiga hatua kubwa. Katika awamu ya kwanza iliyoanza 2023, wanawake 579 nchini Tanzania walipata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na mbinu za biashara. Hii imewawezesha kuongeza mauzo na kipato.
Awamu ya pili, iliyoanza mwaka huu 2025, inalenga kuajiri na kuwafundisha wanawake 500 zaidi katika mikoa mitatu mipya. Pia, wanawake 200 wanapewa mafunzo ya biashara za kidijitali na wanatarajiwa kuuza bidhaa 16,000 za sola, ikiwemo majiko safi 2,000.
Cesear Mloka, Mkurugenzi Mkaazi wa Solar Sister Tanzania, alisisitiza kuwa lengo si tu kuuza bidhaa za nishati, bali ni "kuwawezesha wanawake kujiamini, kupata uhuru wa kifedha na heshima katika familia na jamii zao."
Ushuhuda wa Maisha Bora
Hadithi za mafanikio zinasimama kama ushahidi wa mabadiliko haya. Neema Ally wa Songwe, aliyekuwa akilima mashamba ya watu wengine, sasa ameweza kukodisha ekari tano za ardhi, kulima mahindi, na anaajiri watu wengine kijijini kwake. Vilevile, Theresia John Robert wa Kaskazini mwa Tanzania, aliyekuwa akiponda mawe, sasa amegeuka kuwa mjasiriamali wa sola, akijenga nyumba yake mwenyewe.
Kupitia ushirikiano huu, Solar Sister inalenga kuwafikia watu 85,000 nchini Tanzania kwa bidhaa za nishati jadidifu, hatua itakayopunguza hewa chafuzi na kuboresha afya za kaya. Kama Laura Fruehwald, Meneja wa Programu wa Puma Energy Foundation, alivyosema, nishati safi sasa inatumika kama "kichocheo cha uwezeshaji na maendeleo endelevu," huku Puma Energy ikisaidia kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora na nafuu za kupikia.