Mnazi Bay Kupanua Uzalishaji Gesi kwa Visima Vitatu Vipya

economy | Wed Apr 16 2025


Mnazi Bay Kupanua Uzalishaji Gesi kwa Visima Vitatu Vipya

Katika jitihada za kuimarisha sekta ya nishati nchini, eneo la Mnazi Bay lililoko mkoani Mtwara linatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa gesi asilia. Hii inafuatia mpango wa kuchimba visima vipya vitatu ambavyo vinakadiriwa kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.


Akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara mkoani Mtwara, ziara iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Bwana Hussein Chitemo, ambaye ni Msimamizi wa uzalishaji wa kampuni ya Maurel et Prom Exploration inayoendesha shughuli zake katika eneo la Mnazi Bay, alifahamisha kuwa mchakato wa kuchimba visima hivyo unatarajiwa kuanza kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa 2025.


“Visima hivi vitatu vipya vina uwezo wa kuzalisha zaidi ya futi za ujazo milioni 30 za gesi asilia kwa siku. Kiasi hiki kitaongezwa kwenye uzalishaji wa sasa ambao ni takriban futi milioni 100 zinazotoka kwenye visima vitano ambavyo tayari tunavyo. Mazungumzo na maandalizi yote yanaendelea vizuri na yako katika hatua za mwisho, hivyo tunatarajia kuanza kazi ya uchimbaji kabla ya kufika mwisho wa mwaka huu,” alieleza Bwana Chitemo.


Aliongeza kuwa gesi inayozalishwa kutoka katika visima hivyo husafirishwa kwenda kwenye mitambo ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyoko Mtwara, pamoja na Kituo cha Madimba kinachomilikiwa na GASCO, ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Bwana Chitemo alisema kuwa ongezeko hili la visima vitaweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi katika uzalishaji wa nishati, na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda kutokana na uhakika wa upatikanaji wa gesi asilia.


Naye Mtaalamu wa jiolojia kutoka PURA, Bwana Desmond Risso, alieleza kuwa lengo kuu la mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa sekta ya gesi asilia inakuwa na mchango chanya katika sekta nyingine za uchumi nchini. Alisema kuwa PURA inaongeza juhudi zake kwa kuwekeza katika ushirikiano wa kimkakati na matumizi ya teknolojia za kisasa. Sambamba na hilo, mamlaka inaendelea kuongeza uelewa kwa umma kuhusu sekta hii, na ndio maana wameandaa ziara hiyo kwa waandishi wa habari.


“Tunaamini kwamba vyombo vya habari ni chombo muhimu sana katika kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo fursa zinazopatikana katika sekta ya gesi asilia,” alisema Bwana Risso.


Ziara hiyo ya waandishi wa habari ilihusisha kutembelea miundombinu muhimu kama vile mashamba ya gesi ya Mnazi Bay, Kituo cha Muunganiko wa Bomba la Gesi cha Somanga, na Kiwanda cha Kusafisha Gesi cha Madimba kinachoendeshwa na GASCO. Pia, walitembelea Chuo cha Ualimu Mtwara (K) ambako walishuhudia matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia na mabadiliko chanya yanayoletwa na nishati hiyo.


Bwana Risso aliongeza kuwa kupitia programu ya uelimishaji kwa umma, PURA imekuwa ikiwakutanisha wadau mbalimbali na sekta ya gesi asilia kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi katika kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.


Bi. Joan Ngwale, ambaye ni Ofisa wa Usalama, Mazingira na Uhusiano wa Jamii kutoka kampuni ya Maurel & Prom, alieleza kuwa kuna fursa mbalimbali ambazo wananchi wanaoishi karibu na eneo la uzalishaji wanazipata katika sekta za elimu, afya, na uwezeshaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.


“Tunajenga vyumba vya madarasa kwa ajili ya shule, tunatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, tunajenga vyumba vya kujifungulia kwa akina mama katika vituo vya afya, na tunawawezesha wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi kwa kuwapatia vifaa mbalimbali. Hadi sasa, kuna baadhi ya wanafunzi kutoka maeneo haya wanafanya mafunzo kwa vitendo katika ofisi zetu,” alisema Bi. Ngwale.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.