Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo na wadau muhimu katika sekta ya nishati, akiwemo mwakilishi kutoka kampuni ya Oryx Gas. Katika mazungumzo hayo, wadau hao walimhakikishia Rais kuwa wataendelea kuunga mkono kwa nguvu zote kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuongeza usambazaji wa mitungi ya gesi katika maeneo ya vijijini. Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata gesi kwa urahisi na hivyo kuachana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira, kama vile kuni na mkaa.
Akizungumza katika viwanja vya Jitegemee vilivyopo wilayani Muheza, mkoani Tanga, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kuendelea kuchangia katika juhudi hizi. Aliongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa gesi unakuwa wa uhakika ili wananchi waweze kuitumia bila usumbufu.
"Inapotokea mitungi ya gesi inaisha, mara nyingi inabaki ndani ya nyumba kama samani tu. Hivyo, nimeiomba sekta binafsi kuendelea kusambaza mitungi hii kwa wingi ili wananchi waweze kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia," alisema Rais Samia, huku akiipongeza kampuni ya Oryx Gas kwa jitihada zake katika kuhakikisha gesi inapatikana kwa wananchi.
Kwa upande wake, Meneja Miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kutoka Oryx Gas Tanzania, Peter Ndomba, alieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono kampeni hii kwa kuhakikisha kila kaya nchini inakuwa na mtungi wa gesi ya kupikia.
"Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia. Sisi kama Oryx Gas tumekuwa wadau wakubwa wa ajenda hii na tumeongeza juhudi zetu katika kusambaza mitungi ya gesi hadi katika maeneo ya vijijini," alisema Ndomba.
Aliongeza kuwa kwa sasa mitungi ya Oryx Gas inapatikana katika miji, wilaya, na vijiji vingi nchini. Kampuni hiyo pia inaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuwezesha jamii, hasa wanawake, ili kuwasaidia kubadili mtazamo wao kuhusu matumizi ya nishati ya kupikia. Lengo ni kuhakikisha kuwa wanawake wanakuwa mstari wa mbele katika kutumia nishati safi na salama.
Kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imepata mafanikio makubwa hadi sasa, kutokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali na sekta binafsi. Ushirikiano huu unahakikisha kuwa Watanzania wengi wanapata mbadala wa nishati salama, rafiki kwa mazingira, na yenye manufaa kwa afya zao. Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanasaidia kupunguza uharibifu wa misitu, kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, na kuboresha afya za wananchi.